1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Buhari aiomba Ufaransa msaada dhidi ya Boko Haram

Admin.WagnerD15 Septemba 2015

Rais Francois Hollande wa Ufaransa amesema mapambano ya kulipiga vita kundi la Boko Haram ni sawa na yale dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu kutokana na kwamba makundi hayo yanahusiana.

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria.
Rais Muhammadu Buhari wa NigeriaPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Alamba

Rais Hollande ametowa wito huo wakati akimkaribisha lRais Muhamadu Buhari wa Nigeria katika Kasri la Elysee mjini Paris hapo Jumatatu (14.09.2015) kuanza ziara ya siku tatu nchini humo ambapo anatarajiwa kuomba msaada wa Ufaransa kupambana na kundi la Boko Haram ambapo rais huyo ameonya kwamba kundi hilo la wanamgambo wa Kiislamu wa itikadi kali limezidi kutanuka baada ya kutangaza utii wake kwa kundi la Dola Kiislamu.

Buhari amesema muungano wa makundi hayo uliotagazwa hapo mwezi wa Machi umeipa kundi la Boko Haram chanzo cha kujipatia rasilmali.

Rais Francois Hollande wa Ufaransa amesema wanajuwa kwamba Boko Haram lina mafungamano na kundi la Dola la Kiislamu ambalo kwa lugha ya Kiararabu linatambulikana kama Daesh.

Rais Francois Hollande wa Ufaransa.Picha: Reuters/C. Platiau

Hollande amesema"Kama tunavyojuwa Boko Haram lina mafungamano na Daesh na linapata msaada na kuungwa mkono na kundi hilo. Haiwezekani tena kupambanuwa ugaidi kwa mujibu wa maeneo.Ni ugaidi ule ule unaochochewa na itikadi ya moja ya kifo na ndio sababu kwa nini Ufaransa imeingilia kati nchini Mali."

Kutokomeza Boko Haram

Ziara ya Buhari nchini Ufaransa inakuja miezi mitatu tokea ashike hatamu za kuiongoza Nigeria taifa lenye nguvu kubwa za kiuchumi barani Afrika.

Buhari mwenye umri wa miaka 72 mtawala wa kijeshi wa zamani wa Nigeria pia atakutana na viongozi wa serikali ya Ufaransa katika masuala ya ulinzi,usalama, biasahara na uwekezaji kwa ajili ya nchi yake yenye utajiri wa mafuta.

Buhari ameahidi kulipa kipau mbele suala la kulishinda kundi la Boko Haram tokea aingie madarakani hapo mwezi wa Mei baada ya umwagaji damu wa miaka sita uliosababisha watu 15,000 kupoteza maisha yao na kuwapotezea makaazi wengine zaidi milioni mbili.

Wanajeshi wa Nigeria katika mapambano na kundi la Boko Haram.Picha: picture-alliance/dpa

Wakati wa zaiara hii ya Ufaransa amesisitiza tena umuhimu huo kwa kusema "Ni muhimu kwamba nchi zinazounda Halmashauri ya Bonde la Ziwa Chad kuhakikisha kwamba kufikia mwezi wa Mei mwakani zimelin'gowa kundi la Boko Haram."

Nigeria imeungana na Cameroon,Chad,Niger na Benin kuwa na mkakati wa pamoja wa kulitokomeza kundi hilo la Boko Haram.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman