Buhari apewa ridhaa ya kuliongoza tena taifa la Nigeria
27 Februari 2019Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi amemtangaza Buhari mapema leo kuwa mshindi wa uchaguzi uliocheleweshwa na kugubikwa na kasoro kadhaa za maandalizi pamoja na vurugu. Buhari amemshinda mpinzani wake mkuu Atiku Abubakar, mfanyabiashara na aliyewahi kuwa makamu wa rais. Buhari amejizolea asilimia 56 ya kura akifuatiwa na Abubakar aliyepata asilimia 41 mgombea kutoka chama cha People's Democratic Party PDP.
"Muhammadu Buhari wa chama cha All Progressive Congress, baada ya kufikisha vigezo kwa mujibu wa sheria na kupata kura nyingi, kwahiyo ninamtangaza kuwa mshindi na rais mteule", alisema Mahmood Yakubu mwenyekiti wa tume.
Buhari sasa anakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na kufufua uchumi ambao bado unasuasua kutokana na mdororo wa mwaka 2016 pamoja na mapambano ya kundi la wanamgambo la Boko Haram ambalo limewaua maelfu ya watu huko Kaskazini wengi wakiwa ni raia wa kawaida.
Akizungumza muda mfupi baada ya matokeo kutangazwa ndani ya ofisi za makao makuu ya chama chake cha APC mjini Abuja, Buhari ameahidi kuzidisha juhudi za kuimarisha usalama, kufufua uchumi na kupambana na ufisadi. "Ninawashukuru mamilioni ya Wanaijeria waliopiga kura, walionichagua tena kuwa rais wao kwa miaka minne ijayo. Ninawashukuru sana kwa kuendelea kuniamini kuwatumikia kwa amani".
Hata hivyo mpinzani mkuu wa Buhari, Atiku Abubakar amekataa matokeo ya uchaguzi huo akisema kulikuwa na udanganyifu. Kwenye tamko lake Atiku amesema kwamba "kama ningekuwa nimeshindwa katika uchaguzi huru na ulio wa haki, ningempigia simu mshindi ndani ya sekunde kumueleza kuwa nafahamu juu ya ushindi wako na sio kumpongeza tu, lakini huduma yangu ya kuunganisha Nigeria kama daraja kati ya watu wa Kusini na Kaskazini", alisema mgombea huyo kwenye taarifa yake aliyoitoa kuyakataa matokeo hayo aliyoyaita ya uwongo na kwamba watayapinga kotini.
Waangalizi kutoka Jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS na Umoja wa Mataifa walivitolea wito vyama vyote kusubiri matokeo rasmi kabla ya kutoa malalamiko. Buhari mwenye miaka 76 aliingia madarakani mwaka 2015 ameahidi kupambana na ufisadi na kuboresha mtandao wa miundombinu ya barabara pamoja na reli.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/Ap/Reuters/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu