1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Buhari arejea rasmi Nigeria

20 Agosti 2017

Rais Muhammadu Buhari alirejea nyumbani jana Jumamosi (19 Agosti) baada ya likizo ya miezi mitatu nchini Uingereza alikokwenda kwa ajili ya matibabu kwa maradhi ambayo hadi sasa hayajawekwa wazi.

Nigeria Präsident Buhari Rückkehr
Picha: picture-alliance/Nigeria State House/S. Aghaeze

Akiwa amevalia kanzu nyeusi na kofia, Buhari alionekana akishuka ndege bila kusaidiwa, lakini akiwa ameshikilia njia ngazi ya ndege hiyo baada ya kutua kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abuja.

Alipokelewa na Makamu wa Rais Yemi Osinbajo, ambaye amekuwa akiikaimu nafasi ya urais kwa muda wote kama kiongozi wa mpito, na pia alisindikizwa kwa heshima ya kijeshi. 

Chama tawala cha All Progressive Congress (APC) kilitoa tamko la kuusifia mchango wa Osinbajo, kikisema muda wote ambao Rais Buhari alikuwa nje ya nchi, makamu huyo wa rais "alionesha uongozi uliotukuka hasa kwenye juhudi zake za kuiunganisha nchi na kusimamia kurudi kwa hali ya uchumi wa taifa."

Hata hivyo, Buhari hakutoa kauli yoyote baada ya kushuka ndege na badala yake alichukuliwa moja kwa moja kuelekea kwenye kasri ya rais.

Lakini msemaji wake, Femi Adesina, alitoa taarifa baadaye kwamba Buhari angelizungumza na Wanigeria saa moja asubuhi kwa majira ya Nigeria kesho Jumatatu (Agosti 21).

Likizo ya wasiwasi

Likizo ya Buhari iliyoanza tarehe 7 Mei na iliyokuwa ya pili kwa mwaka huu, aliwaacha wengi nchini Nigeria wakiuliza endapo kweli ana uwezo wa kiafya kuliongoza taifa hilo kubwa kabisa kwa idadi ya watu barani Afrika.

Makamu wa Rais wa Nigeria, Yemi Osinbajo, alikaimu nafasi ya Muhammdu Buhari kwa muda wote kiongozi huyo alipokuwa nje kwa matibabu.Picha: Novo Isioro

Ambapo awamu hii alikaa nje ya nchi kwa zaidi ya siku 100, mapema mwaka huu, Buhari alikuwa amekaa London kwa wiki saba, akisema kuwa aliuguwa ugonjwa ambao hajawahi kuuona maishani mwake, ambapo alizungumzia pia kubadilishwa damu.

Usiri wa maafisa wake kubainisha aina ya ugonjwa anaougua jenerali huyo wa zamani wa kijeshi umezidisha uvumi na wasiwasi. Kumekuwa na sauti kali kutoka upinzani na asasi za kijamii zikitaka ama rais huyo mwenye umri wa miaka 74 ajiuzulu au undani kuhusu afya yake uwekwe wazi.

Katika siku za hivi karibuni, kulikuwa na maandamano katika baadhi ya miji huku waandamanaji wa pande mbili tafauti - wale wanaotaka Buhari ajiuzulu na wale wanaomuunga mkono - wakipambana. 

Wachunguzi wanahofia kwamba kunaweza kuzuka machafuko ya kisiasa nchini Nigeria, hasa upande wa kaskazini unaokaliwa na Waislamu wengi, ikiwa Buhari hataweza kumaliza muhula wake madarakani, ambao unakomea mwaka 2019. Rais aliyemtangulia, Jonathan Goodluck, alikuwa ni Mkristo kutokea kusini kama alivyo makamu wa rais, Osinbajo. 

Hii si mara ya kwanza kwa Nigeria kukumbwa na hali hii, ambapo kiongozi mkuu anabakia muda mrefu nje ya nchi kwa matibabu. Wakati rais wa zamani, Musa Yar'Adua alipokuwa akitibiwa kwa miezi kadhaa ughaibuni kabla ya kurudi nyumbani na kufa mwaka 2009, watu wa kaskazini walimzuwia aliyekuwa makamu wake, Jonathan, kuchukuwa madaraka, hali iliyopelekea mkwamo wa kisiasa kwa muda mrefu.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/dpa/AP
Mhariri: Isaac Gamba
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW