Buhari kurejea nyumbani baada ya matibabu UK
19 Agosti 2017Taarifa kutoka ofisi ya rais ilisema Buhari alietarajiwa kurejea nchini Nigeria Jumamosi jioni baada ya kutibiwa mjini London, atalihutubia taifa kupitia vyombo vya habari vya kielektroniki kufikia saa moja asubuhi siku ya Jumatatu, na kuongeza kuwa kiongozi huyo dhaifu emetoa shukurani zake kwa Wanigeria kwa maombi yao na kumuunga mkono wakati akipata afueni.
Buhari, Jenerali mstaafu alieongoza serikali ya kijeshi mnamo miaka ya 1980, amekuwa akizongwa na uvumi kuhusu hali yake ya kiafya tangu mwezi Juni mwaka uliopita, alipokwenda London kwa mara ya kwanza kwa ajili ya matibabu ya kile kilichoelezwa na wasaidizi wake kuwa maambukizi sugu ya sikio.
Kisha alikaa kwa karibu miezi miwili mjini London Januari na Februari na kusema aliporejea mapema mwezi Machi kuwa hakuwahi "kuumwa namna ile." Mwezi Julai wanachama wa chama chake tawala na wapinzani walikwenda kumuona mjini London na hata wakapiga picha pamoja naye katika juhudi za kutuliza wasiwasi wa umma.
Afya ya viongozi wa Nigeria imekuwa suala nyeti tangu kufia madarakani aliekuwa rais Umar Musa Yar'Adua mwaka 2010, baada ya miezi kadhaa ya kufanyiwa matibabu nje ya nchi.
Wapinzani wakuu wa Buhari katika uchaguzi wa mwaka 2015 uliomuingiza madarakani wamedai kuwa alikuwa na saratani ya tezi dume, madai ambayo mweyewe ameyakanusha.
Waandamanji walitaka arudi au ajiuzulu
Kumekuwepo na mkururu wa maandamano madogo mjini Abuja tangu Agosti 7 kushinikiza Buhari arudi nyumbani au aachie madaraka ikiwa ameishiwa uwezo wa kuongoza. Maandamano hayo yaligeuka ya vurugu wakati wafanyabiashara, wengi wao wakiwa wa kabila la Haussa walipowarushia mawe waandamanaji, na kuwalazimu kuachana na maandamano yao na kutangaza mipango ya kuyahamishia mjini Lagos.
Mmoja wa waandaji wa maandamano hayo Deji Adeyanju, aliliambia shirika la habari la Ufaransa AFP siku ya Jumamosi, kuwa amefurahishwa na habari za kurejea kwa Buhari. "Inamaanisha kuwa lengo letu limetimia na kwamba hatuna nia mbaya na rais," alisema na kuongeza kuwa, " tuliandaa mikutano kumfanya arudi nyumbani ili aendelee kutekeleza majukumu aliokabidhiwa baada ya kuchaguliwa 2015."
Adeyanju alisema maandamano yaliokuwa yamepangwa kufanyika mjini Lagos siku ya Jumatatu yamefutwa. "Hakuna maandamano zaidi kwa sababu rais ameitikia wito wetu. Lakini tutaendeleza kuifuatilia serikali kwa karibu tuwatie mbinyo watekeleze sera nzuri zitakazoshughulikia matatizo mengi yanayowakabili watu," alisema.
Alisema Buhari anapaswa kushughulikia matukio yanayoongezeka ya ukosefu wa usalama nchini kama vile utakeji nyara, mapigano kati ya wakulima na wafugaji, uasi wa Boko Haram na mapambano katika jimbo la Niger Delta.
"Muhimu zaidi, rais anatakiwa kukomesha umaskini mkubwa miongoni mwa raia wengi nchini na mapambano dhidi ya ufisadi yanapaswa kupewa msukumo zaidi," aliongeza.
Imani ya raia kwa Buhari
Dapo Thomas, mwalimu wa siasa katika chuo kikuu cha Lagos alisema kurejea kwa Buhari kutaimarisha mamlaka katika serikali kuu. "Kila sera, kila uamuzi, kila mradi saa utakuwa na mhuri wa mamlaka na uhalali wa kisheria," alisema na kuongeza kwamba kampeni ya kupambana na ufisadi itaimarishwa pia.
"Jambo linalomfanya Buhari akubalike ni uaminifu wake. Ana nia ya dhati ya kuondoa rushwa nchini Nigeria na nadhani kurejea kwake kutaipa msukumo kampeni," alisema.
Buhari, Jenerali mstaafu alieongoza serikali ya kijeshi katika miaka ya 1980, alichaguliwa kuwa rais wa kiraia mwaka 2015 kwa ahadi ya kukomesha rushwa na ufisadi vilivyokithiri katika taifa hilo lenye uchumi mkubwa kabisaa na lenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika.
Dazeni kadhaa za maafisa wa zamani wa ngazi za juu katika serikali iliopita wamekamatwa kuhusiana na tuhuma za rushwa, na kusababisha ukokosoaji dhidi ya madai ya kuwindwa kisiasa.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe, ape, dpae
Mhariri: Yusra Buwayhid