BUJUMBURA: FDD haitokusanya askari kabla ya fedha
5 Januari 2004Matangazo
Kundi kubwa la wapiganaji wa CNDD-FDD, ambalo lilijiunga na serikali ya mpito, limeonya kuhusu uwezekano wa askari wake kuchelewa kufika katika maeneo yao ya mkusanyiko kwa mujibu wa mkataba wa amani ya Burundi uliotiwa saini Novemba iliopita nchini Tanzania. Msemaji wa CNDD-FDD, Kanali Gélase-Daniel NDABIRABE ametaja kuwa tatizo ni pamoja na uhaba wa fedha za kugharamia zoezi hilo na ukosefu wa nia ya kisiasa kwa upande wa serikali. Wafadhili wamekawia hadi sasa kutoa msaada kwa Burundi, inayokabiliwa na vita vya kiraia vya tangu miaka 10 iliopita, ili kuisaidia kutekeleza mkataba huo, ikiwa ni pamoja na gharama za kuwakusanya wapiganaji waliosaini mapatano ya amani. Katika hotuba ya mwaka mpya, Rais NDAYIZEYE alitangaza ratiba ya kazi za kuunda jeshi jipya litakalojumuisha askari wa serikali na FDD, akiwaomba wapiganaji hao kuwa wamewasili katika maeneo yao kabla ya Januari 5. Rais huyo aliahidi pia kuwa shughuli za kuunda uongozi wa pamoja wa jeshi zitakamilika Januari 7 baada ya kamanda wa waasi, Brigedia Adolphe NSHIMIRIMANA kuteuliwa kuwa Naibu mkuu wa jeshi jipya la Burundi mwezi uliopita.