BUJUMBURA: FNL kukutana na Rais wa Burundi
5 Januari 2004Matangazo
Kundi pekee la waasi lililobakia nchini Burundi limesema leo hii litakuwa na mazungumzo ya amani na Rais Domitien Ndayizeye mwezi huu na hiyo kuachana na madai yake ya muda mrefu ya kugoma kukutana na kiongozi huyo na kuondowa muda wa mwisho kwa kasisi mkuu wa Kikatoliki kuondoka katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati iliyoathiriwa na vita. Pasteur Habimana msemaji wa chama cha waasi cha FNL ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba Ndayizeye anataka kuwasikiliza na ameomba kukutana nao na kwa hiyo wamekubali kuzungumza naye kuelezea matatizo yao, mashaka yao na kadhalika na kwamba watakutana naye katika mazungumzo hayo kama baba wa taifa. Amesema mkutano huo utafanyika kati ya Januri 15 na 20 lakini amekataa kutaja mahala utakapofanyika mkutano huo. Zaidi ya watu 300,000 wamepoteza maisha yao tokea mwaka 1993 katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi na makundi yote ya waasi wa Kihutu yaliohusika kwenye vita hivyo isipokuwa FNL yamejiunga na mchakato wa amani na serikali na kujumuishwa serikalini.