BUJUMBURA : Malaika wa Burundi ashinda tuzo ya Umoja wa Mataifa
30 Aprili 2005Matangazo
Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa limetangaza kwamba Tuzo ya Wakimbizi ya Nansen itazawadiwa kwa Marguerite Barankitse anayejulikana kama Malaika wa Burundi.
Tuzo hiyo ambayo inajumuisha medali na dola 100,000 hutolewa kila mwaka kwa mtu au kundi kutokana na huduma zao za kupigiwa mfano katika kuwasaidia wakimbizi.
Baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi Barankitse alianzisha kituo cha kuhifadhi watoto katika mojawapo ya majimbo ya kimaskini kabisa nchini humo.
Katika kipindi cha zaidi ya miaka 12 iliyopita mwanamke huyo amewasaidia zaidi ya watoto 10,000 wa asili ya makabila yote walioathiriwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe pamoja na mizozo mengine katika eneo hilo.