BUJUMBURA : Rajabu aomba hifadhi ubalozi wa Afrika Kusini
23 Januari 2007Kiongozi wa chama tawala nchini Burundi Hussein Rajabu ameomba hifadhi kwenye ubalozi wa Afrika Kusini nchini humo hapo jana kutokana na hofu za usalama baada ya walinzi wake kubadilishwa kwa ghafla.
Akizungumza na radio Bonesha FM Rajabu amesema amekwenda kwenye ubalozi wa Afrika Kusini kwa mashauriano na alipoondoka kwenye ubalozi huo alielezwa kwamba kulikuwa na amri za kutaka kubadilishwa kwa walinzi wake na kutokana na uzoefu wake wa kupigana vita vya chini kwa chini kwa muda mrefu anafahamu amri hizo zinamaanisha nini.
Amesema hatoroki bali atabakia kwenye ubalozi huo hadi hapo hali hiyo itakapoyakinishwa.
Repoti hiyo imekuja masaa machache baada ya mawaziri sita kumtaka Rais Piere Nkurunzinza kuingilia kati katika mzozo wa ndani ya chama tawala cha CNND/FDD ambapo wameonya kwamba unahatarisha kuvuruga amani katika nchi hiyo ilioathirika na vita.
Rajabu analaumiwa kwa masuala kadhaa yaliozusha utata ikiwa ni pamoja na kufunguliwa kwa mashtaka kulikoshindwa dhidi ya Rais wa zamani wa Burundi Domitien Ndayizeye kwa madai ya kula njama ya kuipinduwa serikali.
Burundi ambayo hivi sasa inajaribu kuleta utulivu kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka 13 vilivyogharimu maisha ya watu 300,000 serikali yake hivi karibuni imekuwa ikishutumiwa kwa madai ya kutawala kidikteta na kushindwa kupiga vita rushwa.