BUJUMBURA:Walinda amani wa Umoja wa Mataifa Burundi wataka ufanyike uchunguzi juu ya shambulio la kombora
27 Mei 2005Walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi wametaka kufanyike uchunguzi juu ya shambulio la kombora la hivi karibuni lilosabaisha kujeruhiwa kwa watu watano viungani mwa mji mkuu Bujumbura.
Nureldine Satti Naibu mwakilishi rasmi wa Umoja wa Matifa nchini Burundi amesema hatua hiyo ni muhimu kufanyika kwa ajili ya amani katika uchaguzi unaokuja.
Bwana Satti amesema Umoja wa Mataifa pamoja jumuiya ya Kimataifa haiwezi kukubali uhalifu mwengine wa kivita kutokea katika nchi hiyo na kwa hivyo kundi lolote au mtu yoyote atakayepatikana na hatia ya kuhusika katika uhalifu wa kivita atachukuliwa hatua zinazostahiki.
Ameitaka serikali pamoja waasi wa FNL kushirikiana na wachunguzi wa Umoja huo katika kuwatafuta wahusika wa makosa hayo.
Wanajeshi wa Burundi wamelilaumu kundi la waasi wa kihutu la FNL Kwa mashmbulio hayo ya makombora yaliyofanyika siku ya jummane. Lakini kundi hilo halijasema chochote kuhusu madai hayo.
Waasi na wanajeshi wa Serikali wamepambana mara mbili tangu kiongozi wa FNL Agathon Rwasa na rais Domitien Ndayizeye kutia saini makubaliano ya amani jijini Dares-salam nchini Tanzania mapema mwezi huu.