1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiUlaya

Bulgaria yajiunga na euro: Kwa nini ni jambo kubwa?

29 Desemba 2025

Kujiunga na ukanda wa euro kunaonyesha jinsi uchumi wa Bulgaria ulivyoboreshwa katika muongo uliopita. Hata hivyo, misukosuko ya kisiasa na hasira za wananchi kuhusu usimamizi mbaya wa uchumi na rushwa bado ni changamoto

Sarafu ya euro
Sarafu ya taifa ya Bulgaria, lev, imekuwa imefungamanishwa na euro tangu sarafu hiyo ya euro ilipoanzishwa mwaka 1999.Picha: Wolfgang Filser/Zoonar/picture alliance

Bulgaria inatarajiwa kuanza rasmi kutumia sarafu ya euro tarehe 1 Januari 2026, na hivyo kuwa nchi ya 21 kujiunga na ukanda wa euro. Hatua hii inaashiria mafanikio ya kiuchumi kwa taifa hilo la Ulaya ya Mashariki, lakini pia inakuja wakati wa misukosuko ya kisiasa, hasira za wananchi na wasiwasi kuhusu rushwa na usimamizi mbaya wa uchumi.

Kujiunga na euro ni hatua muhimu tangu Bulgaria ilipojiunga na Umoja wa Ulaya mwaka 2007. Baada ya uamuzi huo, ni nchi sita tu kati ya wanachama 27 wa EU zitabaki nje ya ukanda wa euro: Sweden, Poland, Czechia, Hungary, Romania na Denmark.

Waziri Mkuu wa Bulgaria, Rosen Zhelyazkov, amesema euro "si sarafu tu bali ni chaguo la kimkakati” linaloimarisha nafasi ya Bulgaria barani Ulaya. Kauli hiyo iliungwa mkono na rais wa Bank Kuu ya Ulaya, ECB, Christine Lagarde, aliyesema kuwa kujiunga na euro kutaimarisha misingi ya uchumi wa Bulgaria na kuongeza ushawishi wake katika maamuzi ya kiuchumi ya ukanda huo.

Waziri Mkuu wa Bulgaria, Rosen Zhelyazkov, amesema euro "si sarafu tu bali ni chaguo la kimkakati” linaloimarisha nafasi ya Bulgaria barani Ulaya.Picha: Stoyan Nenov/REUTERS

Je, wananchi wa Bulgaria wanaonaje kujiunga na euro?

Hata hivyo, si Wabulgaria wote wanaoshangilia uamuzi huo. Wapo wanaoamini kuwa kuingia kwenye "klabu ya matajiri” kutaleta maendeleo ya haraka, lakini wakosoaji wanaonya kuwa matarajio hayo yanaweza kuwa ya kupindukia.

Profesa Rossitsa Rangelova wa Chuo cha Sayansi cha Bulgaria anasema kujiunga na euro hakumaanishi moja kwa moja kupanda kwa viwango vya maisha. Anaonya kuwa bila mageuzi muhimu ya muda mrefu—hasa katika taasisi na utawala—Bulgaria haitakuwa mshiriki sawa ndani ya ukanda wa euro.

Sarafu ya taifa hilo, lev, imekuwa ikifungamanishwa na euro tangu mwaka 1999. Bulgaria ilianza rasmi mchakato wa kujiunga na euro mwaka 2018, na mwaka 2020 ikaingizwa kwenye mfumo wa kubadilishana fedha wa Ulaya (ERM II).

Kwa sasa, viashiria vya uchumi vinaonekana kuwa imara. Mfumuko wa bei umeshuka hadi takriban asilimia 2.8 kutoka asilimia 13 mwaka 2022. Nakisi ya bajeti ni karibu asilimia 3 ya pato la taifa, huku deni la taifa likiwa karibu asilimia 24—chini ya viwango vinavyoruhusiwa na EU. Umoja wa Ulaya unatabiri ukuaji wa uchumi wa karibu asilimia 3 mwaka huu, kabla ya kushuka kidogo katika miaka miwili ijayo.

Wafuasi wa mrengo mkali wa kulia wakihudhuria maandamano ya kuilinda sarafu ya Bulgaria, lev, na kupinga kuanzishwa kwa euro, nje ya Benki Kuu ya Bulgaria (BNB) na ofisi ya Uwakilishi wa Tume ya Ulaya. Maandamano hayo yaliandaliwa na chama cha siasa cha mrengo wa kulia mkali na utaifa uliopitiliza cha Revivla mjini Sofia, Bulgaria, tarehe 22 Februari 2025.Picha: Hristo Vladev/Anadolu/picture alliance

Bado kuna safari ndefu ya kufikia kiwango cha EU

Licha ya mafanikio hayo, wachambuzi wanasema Bulgaria bado ina kazi kubwa ya kufanya. Mapato ya wananchi wako karibu asilimia 59 tu ya wastani wa EU, na muundo wa uchumi bado haujafikia viwango vya nchi tajiri za Ulaya Magharibi.

Wataalamu pia wanaonya dhidi ya matumizi makubwa ya serikali baada ya kujiunga na euro, wakitaja hatari ya kurudia makosa yaliyowahi kushuhudiwa katika nchi kama Ugiriki, ambako matumizi ya kupindukia yalichangia migogoro ya kiuchumi.

Changamoto kubwa zaidi huenda isiwe ya kiuchumi bali ya kisiasa. Bulgaria imekumbwa na misururu ya uchaguzi—saba tangu 2021—na bado inakabiliwa na viwango vya juu vya rushwa, kulingana na Transparency International. Hasira za wananchi zimeongezeka kutokana na madai ya usimamizi mbaya wa uchumi na ufisadi serikalini.

Serikali ya Zhelyazkov ilijiuzulu mwezi Desemba kufuatia maandamano makubwa, na uwezekano wa uchaguzi mwingine wa mapema bado upo. Hali hiyo inaweza kudhoofisha imani ya wawekezaji, hasa katika kipindi nyeti cha kuelekea kujiunga na euro.

Wabulgaria wanazidi kukasirishwa na usimamizi mbaya wa uchumi pamoja na rushwa iliyokithiri.Picha: Dimitar Kyosemarliev/AFP

Jamii imegawanyika kuhusu euro

Utafiti unaonyesha Wabulgaria wamegawanyika. Wanaounga mkono euro wanasema itaongeza uwekezaji wa kigeni, kupunguza gharama za kubadilisha fedha na kuimarisha ujumuishaji wa Bulgaria katika soko la pamoja la EU. Wapinzani, kwa upande mwingine, wanaogopa kupanda kwa bei na kupoteza udhibiti wa sera za fedha kwa Benki Kuu ya Ulaya mjini Frankfurt.

Wapo pia wanaodai kampeni za upotoshaji, hasa kutoka Urusi, zimechochea hisia za kupinga euro. Wachambuzi wanasema kujiunga na euro kutaifunga Bulgaria zaidi na Ulaya Magharibi, jambo linaloimarisha Umoja wa Ulaya kwa ujumla.

Kwa ujumla, kujiunga kwa Bulgaria na ukanda wa euro ni hatua kubwa ya kihistoria na ya kimkakati. Lakini wachambuzi wanakubaliana kwamba euro pekee haitoshi kuleta ustawi. Mafanikio ya muda mrefu yatategemea uthabiti wa kisiasa, utawala bora, taasisi imara na sera makini za kiuchumi—vinginevyo, ndoto ya euro inaweza kubaki kuwa ahadi isiyotimia kikamilifu.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW