1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BUNDESLIGA IMENAZA

Ramadhan Ali11 Agosti 2006

Ligi ya Ujerumani-Bundesliga imeanza kwa mpambano kati ya mabingwa Bayern Munich na Borussia Dortmund hapo ijumaa. Duru nyengine ya Champions League-Kombe la klabu bingwa barani afrika iko uwanjani .Mabingwa al Ahly wana miadi na Asante Kotoko jumapili hii.

Picha: AP

Kwa mpambano wa ijumaa baina ya mabingwa watetezi Bayern Munich na Borusia Dortmund katika Allianz Arena,msimu mpya wa Bundesliga ulianza:Munich inacheza msimu huu bila ya Michael Ballack aliejiunga na Chelsea kucheza katika Premier League.

Klabu 3 zimepanda daraja ya kwanza msimu huu-Allemania Aachen yenye miadi leo na Bayer Leverkusen,Energie Cottbus-timu pekee kutoka Ujerumani Mashariki inayopambana wakati huu na Borussia Moenchengladbach na Bochum inayopapurana wakati huu na Mainz.

Jumapili,Hannover inakumbana na makamo bingwa Werder Bremen ambayo mwishoni mwa wiki iliopita iliizaba Bayern munich mabao 2:0 na kutwaa Kombe la Ligi la Ujerumani lionaloaniwa kabla msimu wa Bundesliga kuanza.

Mpambano mwengine kesho ni kati ya Wolfsburg na Hertha Berlin.

Klabu 3 zilizoteremshwa daraja ya pili kutoka ya kwanza ni FC Cologne,ambayo imebidi kumuuza jogoo lake Lukas Podolski kwa mabingwa Bayern Munich.Nyengine ilioteremka na Duisburg na Kaiserslauten.

KOMBE LA KLABU BINGWA BARANI AFRIKA:

Uhasama mkubwa unaanza tena jumapili pale wenyeji Asante kotoko ya Ghana ,wanapo wakaribisha mabingwa wa kombe la klabu bingwa barani Afrika-Al Ahly ya Misri.Majogoo hao wa Kumasi na mashetani wekundu wa Kairo, wamepambana mara mbili katika finali ya Kombe hili n amara moja katika nusu-finali.Al Ahly mara nyingi ikitamba.

1982 Al Ahly ilishinda kwa mabao 4:1 baada ya duru zote mbili kufuatia kuongoza kwa mabao 3 duru ya kwanza.Lakini katika duru ya pili ,walikomewa bao 1:0.Katika kinyan’ganyiro cha taji la 1987,Al Ahly iliitoa Asante Kotoko kwa mabao 2-1 ikiwa njiani kuelekea finali.

Wakati Al Ahly ililitwaa kombe 2001,Kotoko haikufua dafu nyumbani na barani africa.Kotoko ililazwa katika finali ya 1993 na Zamalek ya Misri.

Ikapata pigo jengine katika finali ya Kombe la CAF-shirikisho la dimba la Afrika, ilipopokonywa kombe na wenzao Hearts of Oak.

Lakini, mla , ni mla leo, mla kesho kala nini ?

Changamoto hii ya mechi 4 mwishoni mwa wiki hii kwa keli inaanza jioni hii mjini Johannesberg ambako Orlando Pirates ya africa Kusini lazima iitie munda Hearts of Oak ili inusuruke na kubaki mashindanoni na kuwa na nafasi katika moja ya nusu-finali 2.

Pirates, klabu pekee ya AKusini, kutwaa Kombe la klabu bingwa barani Afrika, ilimudu sare tu nyumbani na ASEC Abidjan ya Corte d’Iviore.

Mabingwa wa mwaka juzi Enyimba ya Nigeria,hawabashiriki .Walitamba huko Ghana walipoikumta Hearts of Oak mabao 2:0,lakini walipocheza nyumbani walibidi kutoka nyuma kuizuwia Pirates isio na maarifa ya kutosha.Hapo kabla ililazwa na ASEC mabao 4:1.

Ama katika changamoto za kombe la Shirikisho la dimba la africa, InterClub ya Angola ina miadi leo na Petro Atletico pia ya angola.

Mjini Rabat, FAR-mabingwa wanaumana na Esperence ya Tunisia.

Na mjini Lumbubashi St. Loi Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya kongo inakutana na Renacimiento.

Stadi wa Ufaransa, Thiery Henry ametangaza kwamba hana nia ya kufuata nyao za Zinedine Zedane na kustaafu na anatumai kuiongoza Ufaransa katika kombe la kwanza la dunia barani Africa 2010.

Nahodha huyo wa Arsenal, atakua na umri wa miaka 32 pale Kombe hilo la dunia litakapoaniwa Africa Kusini.”Kwanza tutakuwa na kombe la Ulaya la Mataifa 2008.Na halafu kwenda Afrika kusini,itafurahisha sana.”

Henry ana matumaini mema kwamba, Ufaransa yaweza kuegemea mafanikio yake nchini Ujerumani wakati wa kombe la dunia ,lakini alionesha hadhari ichukuliwe katika kinyan’ganyiro kinachokuja cha kuania tiketi za kombe la Ulaya la mataifa litakalochezwa Uswisi, 2008.Ufaransa itaanza changamoto zake kwa mpambano na Georgia,Septemba 2.

Katika mashindano ya riadha ya ubingwa wa Ulaya mjini Gothenburg,Sweden, Francis Obikwelu,mzaliwa wa Nigeria, anaekimbia chini ya bendera ya Ureno,

alitamba kati ya wiki hii alipoibuka na mataji 2- katika mita 100 na jengine mita 200.Hivyo, Obikwelu, amekuwa mwanariadha wa kwanza tangu Pietro Mennea wa Itali,1978 kutwaa mataji hayo. Na hakuna shaka sasa kwamba, Obikwelu ndie menda mbio wa kasi barani Ulaya.Obikwelu alichukua uraia wa Ureno, 2001.

Ringi ya mabondia itatikisika leo usiku pale mbabe wa wezani wa juu ulimwenguni ,muamerika mzaliwa wa Ksakhstan, Oleg Maskaev akijitosa ringini kujaribu kuzoa mataji yote 3 ya wezani huo wa juu duniani.

Hasimu yake usiku wa leo ni bingwa wa taji la WBC-world Boxing council,Hasim Rahman.Mwanajeshi huyo wa zamani wa Urusi,Maskaev alichukua uraia wa Marekani miaka 2 nyuma na usiku wa leo-anadai mramba asali,harambi mara moja:kwani alikwisha mkandika magmi hasim Rahman, 1999 na kumpiga kumbo.

Walipopima wezani wao kabla changamoto ya leo usiku, Maskaev alikuwa na uzito wa pauni 238,pauni 3 mzito zaidi kuliko Rahman.Maskaev ameshinda mapambano 10 mfululizo na katika ushindi wake wa siku za mwsanzo ni pale alipomtia rimuri-muri Rahman na kumpiga kumbo katika duru ya 8, 1999.

Rahman ana sifa ya ushindi mara 33 na mara 2 sare na anakumbukwa kwa kumtandika Lennox Lewis duru ya 5 huko Afrika Kusini.

Muandazi wa mabondia,Bob Arum, anajaribu kupanga miadi ya mutano ringini April mwakani kati ya Hasim Rahman na kiltchko hadi ifikapo april, mwakani.

Bingwa wa zamani wa mabondia mzee Joe Frazier,(62) amehuzunishwa kuona ringi ya mabondia ya kisasa ya wezani wa juu ulimwenguni haitambi.Alidai mabondia hawaongozwi sawa sawa katika mitindo ya kile0 ya mafunzo.Alisema, “Vijana hawa hawafanyi mazowezi ipasavyo.”

Frazier alikosoa pia mtindo wa kuwapo mashirika mengi ya mabondia .Frazier, alikuwa bingwa wa dunia wa wezani wa juu kwa miaka 3 mnamo miaka ya 1970ini kabla hakupigwa kumbo na Gorge Foreman na kupokonywa taji.Frazier alipata umaarufu kwa changamoto zake 3 na mbabe wa wababe-Muhammad Ali.Alishinda changamoto ya kwanza na akashindwa mbili zilizofuata.Yatatu ilikua mjini Manila.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW