Bundesliga kuanza rasmi Ijumaa
14 Agosti 2017Bundesliga inaanza kutimua vumbi siku ya Ijumaa tarehe 18 kwa pambano kati ya mabingwa watetezi Bayern Munich na Bayer Leverkusen katika uwanja wa Allianz Arena. Lakini nini kinachotarajiwa mara hii katika msimu huu wa 55 wa Bundesliga, ambapo timu zinazoonekana kuwa na utamaduni wa kushika nafasi za juu kama Schalke 04, Bayer Leverkusen , Borussia Moenchengladbach zimeporomoka na hata hazimo katika mashindano ya ligi ya Europa, mara hii.
Kwa upande wa tetesi za kuhama wachezaji , tetesi kumhusu Ousmane Dembele wa Borussia Dortmund hazija muacha salama. Kila siku tetsi hizo zinazidi kuongezeka akihusishwa na kuhamia FC Barcelona ya Uhispania. Dembele kutokana na utovu wa nidhamu ambapo alishindwa kufika katika mazowezi ya timu hiyo siku ya Alhamis ameadhibiwa kwa kuondolewa katika kikosi cha kwanza na atakaa nje ya kikosi hicho hadi mwishoni mwa mwezi huu.
Dembele amefanya hivyo akitaka kutoa mbinyo kwa timu yake kumruhusu kwenda kuchezea Barcelona. Barcelona wametoa kiasi cha euro milioni 90 pamoja na malipo mengine ya bonasi hapo baadae kuweza kumpata mchezaji huyo chipukizi mwenye umri wa miaka 20, raia wa Ufaransa. Lakini Dortmund wamekataa wakitaka kitita cha euro milioni 140 hadi 150 ili kuweza kumuachia mchezaji huyo.
Barcelona yatakiwa kusajili wachezaji wapya
Barcelona inalazimika kusajili wachezaji wapya , amesema mchezaji wa kiungo wa timu hiyo Sergio Busquets , na timu hiyo inawania kuwasajili Ousmane Dembele wa Borussia Dortmund na Philippe Coutinho wa Liverpool ili kuimarisha kikosi chake kilichoondokewa na mchezaji nyota Neymar ambaye ametimkia Paris St. Germain kwa kitita cha milioni 222.
Baada ya Barcelona kutwanga mabao 3-1 na mahasimu wao wakubwa Real Madrid jana Jumapili katika kombe la Super Cup , linaloashiria kufungua msimu wa ligi ya Uhispania , tayari imechukua hatua ya kukiimarisha kikosi chake na wamepata saini ya mchezaji wa kiungo Paulinho kutoka klabu ya Guangzhou Evergrande kwa kitita cha euro milioni 40 , klabu hiyo imethibitisha leo.
Barcelona inaelekea mjini Madrid kupambana na Real Madrid katika mkondo wa pili wa kinyang'anyiro cha kombe la Super Cup huku ikiwa na matumaini finyu ya kuweza kurejesha mabao hayo, licha ya kuwa mshambuliaji hatari wa Real Madrid Cristiano Ronaldo hatakuwamo katika kikosi hicho kutokana na kupewa kadi nyekundi katika mchezo huo. Hata hivyo kocha wa Real Zinedine Zidane amesema klabu yake itafikiria kukata rufaa kwa uamuzi huo katika shirikisho la kandanda la Uhispania kupinga kadi ya pili ya njano dhidi ya Ronaldo.
TSG Hoffenheim yaikabili Liverpool
TSG Hoffenheim ya Ujerumani inakutana na FC Liverpool ya Uingereza katika mkondo wa kwanza wa mchezo wa mchujo wa kuwania kufika katika awamu ya makundi ya Champions League barani Ulaya , na kufikia kilele cha safari yao inayoonesha mafanikio makubwa kwa timu hiyo ya kijijini Sinsheim , nchini Ujerumani. Hoffenheim na Liverpool zina historia tofauti kabisa na vigogo hao barani Ulaya wako katika historia tofauti kabisa wakati wakiingia katika awamu hii ya mchujo ya kombe hilo.
Liverpool ni mabingwa mara tano wa kombe hilo wakati Hoffenheim ndio kwanza wanaonja mikiki mikiki ya kinyang'anyiro hicho, baada ya kumaliza katika nafasi ya nne katika Bundesliga msimu uliopita.
Lakini katika kikosi cha kocha Jurgen Klopp wa Liverpool mchezaji mmoja anakosekana. Philippe Coutinho ameachwa nyumbani , bila shaka kutokana na majadiliano ya kutaka kujiunga na Barcelona ya Uhispania.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe /dpae / ape / rtre
Mhariri: Mohammed Khelef