1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bundesliga kurejea bila mashabiki viwanjani

3 Januari 2022

Kivumbi cha kandanda la Ujerumani – Bundesliga kinaanza tena kutimuliwa Ijumaa hii 08.01.2022, ikiwa ni katika duru ya pili ya msimu bila mashabiki uwanjani kutokana na ongezeko la maambukizi

Fußball FC Bayern | Symbolbild
Picha: Kerstin Joensson/AFP/Getty Images

Kuna wasiwasi mkubwa wa kuongezeka kwa maambukizi hasa baada ya vilabu vingi kutangaza kuwa wachezaji wao wamepatikana na maambukizi baada ya kurejea mazoezini kutoka mapumziko mafupi ya msimu wa baridi.

Miongoni mwa vilabu hivyo ni Bayern Munich (5), RB Leipzig (3), Wolfsburg, Borussia Monchengladbach, Stuttgart (5). Bado hata hivyo haijulikani kama hali itakuwa mbaya kama inavyoshuhudiwa katika Premier League ambako mechi inabidi ziahirishwe.

Donata Hopfen mkuu mpya wa DFLPicha: DFL/dpa/picture alliance

Na mtu atakayekuwa katika mstari wa mbele katika kufanya maamuzi hayo, ndio kwanza tu amechukua usukani. Bi Donata Hopfen amekuwa mwanamke wa kwanza kusimamia kandanda la Bundesliga. Alichukua usukani tarehe mosi mwezi huu kutoka kwa Christian Seifert wa kuwa mkuu wa DFL, kitengo ambacho kinasimamia shughuli zote za Bundesliga.

Seifert anaondoka baada ya miaka 17 uongozini na kuisaidia Bundesliga kuwa mojawapo ya mashindano yanayotambulika Zaidi ya kandanda duniani na hata kumudu kipindi kigumu cha janga la corona kuliko wengine walivyofanya.

Mrithi wake, Bi Hopfen mwenye umri wa miaka 45 ana mambo kadhaa yanayomsubiri ikiwemo kuyarekebisha mahusiano na chama cha kandanda Ujerumani – DFB na pia kusimamia ligi wakati huu wa corona. Sio mtu anayefahamika sana katika usimamizi wa mambo ya kandanda lakini kutokana na uzoefu wa mambo ya kiditijali na kimkakati kwa hivyo anaungwa mkono kufanya vyema.

Tukirudi uwanjani, Bayern watalenga kuendeleza walikioachia Desemba, wakilenga kubeba taji lao la 10 mfululizo. Watashuka dimbani Allianz Arena Ijumaa kucheza mechi ya 18 ya msimu dhidi ya Borussia Moenchegladbach.

reuters, dpa, ap, afp

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW