Bundesliga: Mapambano dhidi ya kushuka daraja wiki hii
8 Machi 2014Na baadhi ya timu hizo zinakabiliana . Hamburg SV kwa mfano ina miadi na Eintracht Frankfurt. Ikiwa na points 19 tu katika nafasi ya 16 Hamburg maji yamewafika shingoni.
Huko Uingereza Manchester inaelekea West Bromwich Albion leo jioni kuanza kipindi ambacho kitaamua hatima yao katika msimu huu uliojaa matatizo.
Klabu ya Hamburg SV ambayo ni kongwe katika bundesliga , ikiwa na kocha mpya Mirko Slomka inaweza tu kuwa na matumaini , kwamba Eintracht Frankfurt baada ya kocha wake mkuu Armin Veh kutangaza kuwa hatakuwa kocha wa timu hiyo msimu huu utakapomalizika , kuwa kutakuwa na hali isiyokuwa tulivu katika kikosi hicho jioni ya leo(08.03.2014).
Timu hiyo inakabiliwa hata hivyo na balaa la majeruhi kwa wachezaji wake muhimu. Hamburg haitakuwa na mlinzi wake muhimu Marcel Jansen aliyeumia wakati akitumikia kikosi cha timu ya taifa katika mchezo wa kirafiki na Chile katikati ya wiki hii, pamoja na mshambuliaji wao Michel Lasoga ambaye pia aliumia wakati akiwa katika kikosi cha timu ya taifa . Mirko Slomka amezungumzia mchezo wa leo jioni.
"Hatutaki kujificha katika balaa la majeruhi na pia kuanza kulalama. Tunaendelea kuwa na matumaini , tunacheza nyumbani, na pia tuna wachezaji wengi katika kikosi chetu ambao wanaweza kuchukua nafasi hizo. Kwa hiyo bado naamini , kwamba tunaungwa mkono na mashabiki wetu katika mchezo huu."
Hannover 96 ambayo kama Hamburg imezongwa na matatizo kadha pamoja na kujikusanyia points 25 , inasafiri kwenda mjini Leverkusen kupambana na timu ambayo nayo imetumbukia katika matatizo ya Bayern .
Kocha wa Hannover Tayfun Torkut anatambua kuwa kikosi cha Bayer Leverkusen kina uwezo mkubwa na inabidi wajaribu kadri ya uwezo wao kuizuwia Leverkusen kuingiza madhara zaidi katika kikosi hicho jioni ya leo.
Mpambano ambao unaangaliwa zaidi jioni ya leo ni wa majirani katika msimamo wa ligi ambao piga ua ni lazima mmoja wao ashinde ili kujiweka katika njia salama ya kuepuka kushuka daraja ni kati ya Nürberg na Werder Bremen. Nürnberg iko katika nafasi ya 14 wakati Bremen inashikilia nafasi ya 13 zikiwa na points 25 zote.
Kocha mkuu wa VFB Stuttgart hata hivyo anajikuta katika mbinyo mkubwa zaidi. Thomas Schneider kiti chake kinayumba. Iwapo Stuttgart itaanguka dhidi ya Eintracht Braunschweig, kichwa chake kitakuwa halali kwa viongozi wa timu hiyo. Itakuwa kipigo cha tisa kwa timu hiyo Schneider akiwa kocha. Fredi Bobic ni mkurugenzi wa spoti wa Stuttgart.
"Utakuwa kama mchezo wa fainali, na hili linaeleweka. Lakini pamoja na hayo, tunataka kushinda mchezo wa leo Jumamosi na kisha tunataka mchezo wa Jumamosi ijayo tushinde. Hilo ndio lengo letu. Tumo katika mpambano wa kujinasua kutoka kushuka daraja na hakuna kitu kingine muhimu hivi sasa, kama kuelekeza nguvu zetu katika mchezo unaokuja."
Bayern Munich itakuwa nyumbani ikiikaribisha VFL Wolfsburg , na Schalke 04 iko nyumbani ikiisubiri 1899 Hoffenheim. Borussia Moenchengladbach inajaribu tena bahati yake kutafuta njia ya kujitoa katika gea ya kurejea nyuma, mara hii ikipambana na FC Augsburg.
Jumapili(09.03.2014) Borussia Dortmund itakuwa ugenini ikipambana na Freiburg na pia Mainz 05 ina miadi na Hertha BSC Berlin.
Huko Uingereza katika premier League Manchester United ambayo imekabiliwa na msimu wenye matatizo kadha msimu huu wanaelekea West Bromwich Albion katika pambano ambalo litakuwa mwanzo wa kipindi cha kuamua nini hatima yao msimu huu.
Viongozi wa ligi hiyo kwa sasa Chelsea inamiadi na Tottenham Hotspurs wakitaraji kuongeza mwanya uongozi hadi points saba iwapo itaishinda timu hiyo. Kipigo cha Arsenal London dhidi ya Stoke City mwishoni mwa juma lililopita , na Manchester City ikishiriki katika fainali ya kombe la ligi ilisababisha Chelsea kuweka mwanya wa points 4 na ushindi dhidi ya Spurs utaimarisha nafasi ya kikosi hicho cha kocha Jose Mourinho.
Kwingineko Norwich itakuwa wenyeji wa Stoke City, wakati Southampton inaitembelea Crystal Palace.
Nchini Uhispania , Barcelona inaweza kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi wakati ikifanya ziara huko Valladolid leo jioni. Huku Real Betis ikiikaribisha Getafe, Celta Vigo ina miadi na Atletico Madrid na Granada iko nyumbani ikiisubiri Villarreal. Real Madrid inakumbana na Levante kesho Jumapili (09.03.2014).
Mwandishi: Kops , Calle / ZR / afpe / rtre / Sekione Kitojo
Mhariri: Josephat Charo