BUNDESLIGA NA SOKO LA WACHEZAJI WAPYA
1 Agosti 2005
Bundesliga-Ligi ya Ujerumani inaanza msimu mpya mwishoni mwa wiki hii ijayo na kama msimu uliopita,klabu 2 hasa zimejiimarisha kwa kununua wachezaji wengi wapya:mabingwa Bayern Munich kutoka kusini na Hamburg SV kutoka kaskazini.Hata Werder Bremen haikukaa nyuma katika kinyan’ganyiro cha soko la wachezaji kabla msimu kuanza.Kwa jumla, klabu 18 zinazoshiriki katika Bundesliga zimetumia kitita cha Euro milioni 71 na klabu 5 kati ya hizo pekee zimetumia thuluthi-mbili ya fedha hizo kwa wachezaji.
Klabu zenyewe ni Munich,Hamburg,Bremen,Schalke na Stuttgart ambazo kwa jumla zimetumia kiasi cha euro milioni 50 kama raslimali kwa wachezaji wapya msimu mpya.
Mabingwa Bayern Munich ambao mwishoni mwa wiki waliilaza jubilo Iwata ya japan kwa mabao 3-1 –mawili akitia Michael Ballack,ilitumia kitita kikubwa kumuajiri mlinzi mfaransa Valerien Ismael kutoka werder Bremen.Walilipa kima cha Euro milioni 8.
Isitoshe, Munich imemfungisha mkataba Muiran Ali Karimi-mchezaji bora wa dimba barani Asia wakati huu na amekuwa akiitwa “Maradona wa Asia”.
Hamburg imetupa mshipi na kumvua mchezaji wa kiungo Rafael van der Vaart kutoka Ajax Amsterdam. Rafael alitakiwa pia na Manchester United na hata Juventus.Hamburg ilimkomboa kwa kitita cha Euro milioni 5.1.Hamburg imemvua pia simba wa nyika Timothee Atouba kwa kitita cha euro milioni 2.5 kutoka Tottenham Hotspur.
Ama Schalke 04 –mahasimu wakubwa msimu uliopita wa mabingwa Bayern Munich wamemnyakua mshambulizi hatari Kevin Kuranyi kutoka Stuttgart kwa kitita cha Euro milioni 7.
Kocha mpya wa Stuttgart, mtaliana Giovanni Trapattoni, amemuajiri Jon Dahl Tomasson kutoka AC Milan kwa kima cha Euro milioni 8.
Borussia Dortmund ambayo imeishiwa na fedha wamutupa mshipi na mapema na kumuajiri wingi kutoka Africa Kusini Delron Buckley kwa kima cha Euro 425,000 kutoka klabu ya Bielefeld alikohamia kutoka Bochum.
Klabu 3 zilizorejea daraja ya kwanza ya Bundesliga msimu huu mpya-FC Cologne,Frankfurt na Duisburg,zimetumia fedha nyingi zaidi kupita Dortmund.
NJE YA BUNDESLIGA:
Mabingwa wa Ligi ya uingereza Chelsea walikamilisha ziara yao ya Amerika kaskazini jana kwa kuondoka suluhu bao 1:1 na AC Milan ya Itali huko New Jersy.Mnamo dakika ya 10ya mchezo mkwaju mkali wa Cafu nusra unase katika lango la Chelsea. Kabla kipindi cha pili , Didier Drogba wa Ivory Coast aliipatia bao Chelsea baada ya kuwachenga walinzi 3 wa Milan.Mnamo dakika ya 80 ya mchezo Manuel Rui costa alisawazisha bao hilo.
Luis Figo wa Real Madrid yabainika hataitikia hodi hodi za FC Liverpool,mabingwa wa Ulaya na yamkini, akafunga mkataba na Inter Milan.
Real yadhihirika imeshaafikiana na klabu ya Santos ya Brazil kumuajiri stadi chipukizi Robinho kwa kima cha Euro milioni 30.Katika mtandao wa Real waliarifu mwishoni mwa wiki kwamba, Robinhno atajiunga nao hapo August 25 baada ya kukamilisha mechi 5 na klabu yake ya sasa Santos huko Brazil.Kuwasili kwa Robinho mjini madrid, kutazusha wasi wasi katika hali ya muingereza Michael Owen, ambae anasemekana kunuwia kurejea katika Premier League-Ligi ya Uingereza.
Bingwa wa rekodi ya dunia wa mita 100 Asafa Powell sasa ni wazi kabisa hatakimbia katika mashindano hayo ya ubingwa wa dunia mjini Helsinki yanayoanza jumamosi hii ijayo.Isitoshe, wanariadha wengi wa Kenya wanaendelea kupepea bendera za nchi tajiri za ghuba na kuhatarisha kikapu chao cha medali.
Katika Changa moto ya mataifa 3 ya RUGBY:
Wenyeji Afrika Kusini-Springboks walitamba jumamosi kwa mabao 22-16 dhidi ya mahasimu wao wakubwa Australia.Hivyo wameanza vyema kabisa kutetea taji lao.
/