1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bundesliga; Stuttgart yapokea kipigo cha pili mfulizo

6 Novemba 2023

Mwanzo mzuri wa VfB Stuttgart kwenye Bundesliga msimu huu umekwama tangu mfungaji wao bora Serhou Guirassy kuumia.

Deutschland Bundesliga Heidenheim gegen VfB Stuttgart
Mechi kati ya Heidenheim na StuttgartPicha: Eduard Martin/Jan Huebner/IMAGO

Imepoteza mara mbili mfululizo. Hapo jana walipokea kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya timu iliyopanda daraja Heidenheim.

Soma pia: Pigo kwa Stuttgart, Guirassy nje kwa wiki kadhaa

Jan Schöppner wa Heidenheim alitia kimyani bao la kwanza kunako dakika ya 70, huku Tim Kleindienst akifunga mchezo kwa kuwaduwaza Stuttgart katika uga wa Voith-Arena.

Licha ya kipigo hicho Stuttgart wamesalia katika nafasi ya tatu kwenye jedwali, pointi saba nyuma ya viongozi wa ligi Bayer Leverkusen na tano nyuma ya mabingwa watetezi Bayern Munich katika nafasi ya pili.

Wolfsburg na Werder Bremen zilitoka sare ya 2-2 na kuhitimisha msururu wa vichapo kwa wenyeji na kuwapa wageni pointi ya kwanza wakiwa ugenini msimu huu.

Tuchel mwamba wa mbinu 

Kocha wa Bayern Thomas TuchelPicha: Ulmer/Teamfoto/IMAGO

Katika mechi yengine, Ustadi wa kocha Bayern Munich Thomas Tuchel ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu katika derbi ya Klassiker na bila shaka aliondoa mashaka miongoni mwa wafuatiliaji wa soka, na kufuta rekodi ya Dortmund chini ya kocha Edin Terzić ya kutofungwa kwenye Bundesliga tangu mwezi Aprili.

Kwa kutumia mfumo wake wa kawaida wa 4-2-3-1 Dortmund walikiona cha mtema kuni kwani Tuchel alikuwa na kadi ya siri iliyoipa ushindi mnono ugenini Signal Iduna Park.

Baada ya mechi Edin Terzićalisema "Kimsingi kila tulilojaribu kulizuia tulijaribu kulikwepa tuliliacha litokee; tulianza kwa kusuasua tulipoteza mipira mingi sana, tuliruhusu goli kwa kona ya kwanza na hili ni jambo ambalo linatuudhi sana. Haswa katika kiwango hiki, ikiwa utakubali kufungwa mapema, itakuwa vigumu kurudi kwenye mchezo. Kisha tukapoteza mipira mingi, haswa katika eneo la adhabu na tukafungua mazingira mengi kwa mashambulizi ya kushtukiza. Kimsingi, mechi ilianza tukiwa chini kwa 2 bila."

Mfalme wa mabao Harry Kane alitawala tena kwa kutia kimyani mabao matatu kwa mara ya tatu tangu alipojiunga na Bayern Munich. Kane ana jumla ya mabao 15 katika mechi 10 alizocheza za Bundesliga. Serhou Guirassy wa Stuttgart anafuata kwa mabao 14 katika mechi 8 na amekosa mechi mbili kutokana na jeraha. Winga Leroy Sane amecheka na wavu mara 8 katika mechi 10  idadi sawa ya magoli na Loïs Openda wa RB Leipiz na Jonas Wind mshambuliaji wa Wolfsburg.

Harry Kane ana kila sababu ya kusherekea. "Lazima niendelee kufanya ninachofanya. Nilisema wiki iliyopita, nikiwa na wachezaji hawa karibu yangu, najua nitapata nafasi kwa hivyo lazima niwe mahali pazuri. Kwa kweli nafurahia sana kuwa hapa. Tuendelee tu. Ushindi wa ugenini ni muhimu ni Usiku mzuri sana." Alisema baada ya mchezo dhidi ya Dortmund.