Bundesliga yaingia katika mchezo wa nne
22 Septemba 2012Hamburg SV, ambayo hadi sasa haijapata point katika bundesliga, yaapa kuwachafulia mabingwa wa ligi hiyo, Borussia Dortmund, rekodi yao ya kutoshindwa katika michezo 31 ya ligi. Huko Uingereza katika Premeir League , Liverpool na Manchester United kupimana ubavu leo.
Mchezo mkubwa wiki hii , au "Big Match", utakuwa huko mjini Gelsenkirchen leo jioni wakati makamu bingwa wa ligi ya Ujerumani, Bundesliga , Bayern Munich itakapopimana ubavu na Schalke 04.
Kinachoangaliwa katika mchezo huo ni iwapo mchezaji wa kati kutoka Uholanzi, Ibrahim Affelay, ataweza kuipa Schalke 04 maarifa zaidi ya kuweza kufanya mashambulizi dhidi ya Bayern Munich.
Arjen Robben, ambaye alionyesha mchezo mzuri dhidi ya Valencia katika pambano lao la Champions League ameonyesha kuiheshimu Schalke.
Pamoja na hayo anataka kuingia uwanja leo jioni kuonyesha uwezo wa timu hiyo na kushinda mchezo huo.
Hamburg SV, ambayo haijashinda mchezo hata mmoja kati ya michezo mitatu iliyokwishacheza katika Bundesliga hadi sasa, imeapa kuichafua rekodi ya mabingwa watetezi Borussia Dortmund ya kutofungwa katika michezo 31 ya ligi hadi sasa tangu msimu uliopita.
Borussia Dortmund inaingia katika mchezo huo ikiwa kifua mbele baada ya ushindi katika mchezo wao wa kwanza katika Champions League msimu huu dhidi ya mabingwa wa uholanzi, Ajax Amsterdam, kwa bao 1-0.
Nahodha wa Hamburg, Heiko Westermann, ameonyesha kuwa hakuna kilichobadilika , wakati aliposema , kuwa timu yake ina wachezaji wenye uwezo , ambao unaweza kuiangusha timu yoyote ile.
Fortuna Dusseldorf hadi sasa haijaonja kipigo licha ya kurejea kwa mara ya kwanza katika kiwango hiki cha ligi baada ya miaka kadha katika ligi daraja la pili. Wapinzani wa Fortuna Dusseldorf mara hii ni Freiburg , ambayo imepata ushindi mara moja na kutoka sare mara mbili.
Tunataka katika mchezo huu kuweka muhuri wetu katika ligi, amesema hivyo kocha wa Freiburg , Christian Streich.
VFL Wolfsburg inaikaribisha Greuther Fürth. FSV Mainz inakabana koo na majirani zao katika msimamo wa ligi FC Augsburg. Vilabu vyote hivyo katika hali waliyonayo hivi sasa hawataridhika na kugawana point. Chechefu mmoja kati yao anaweza kubadili hali hiyo.
Michezo mitatu itafanyika siku ya jumapili. Kutokana na timu tatu za Bundesliga kuwamo katika kinyang'anyiro cha Europa League siku ya Alhamis, timu hizo zimepewa muda wa kupumzika kidogo kabla ya kuingia katika Bundesliga.
Leverkusen ina miadi na Borussia Moenchengladbach, Bremen inaumana na Stuttgart na Hoffenheim ina matumaini ya kubadili majaliwa yake kwa kuwa hadi sasa imeshindwa kuambulia hata point moja na inaumana na Hannover.
Kasheshe Premier League
Na katika Premier League, mchezaji wa kiungo Michael Carrick, ameomba mashabiki wa Manchester United kuwa watulivu wakati timu hiyo itakapopambana na mahasimu wao wakubwa, Liverpool, katika pambano ambalo litakuwa na mhemko mkubwa uwanjani Anfield kesho Jumapili.
Ziara ya Manchester United katika uwanja wa Anfield huwa kwa kawaida na hali ya hisia kali kutokana na uhasama mkubwa baina ya mashabiki wa vigogo hao wa soka la Uingereza.
Michezo mingine siku ya jumapili (23.09.2012) ni kati ya Newcastle ambayo inapambana na Norwich City, Manchester City inapimana nguvu na Arsenal na Tottenham Hotspurs inagaragazana na Queens park Rangers.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / rtre /
Mhariri: Othman Miraji