Bundesliga yarejea tena uwanjani
25 Januari 2016Ligi ya Ujerumani Bundesliga imerejea uwanjani Ijumaa iliyopita , wakati Bayern Munich ilipokuwa wageni wa Hamburg SV na kurejea mjini Munich na pointi, tatu baada ya kuishinda Hamburg kwa mabao 2-1.
Bayern Munich inaelekea kuwa klabu ya kwanza kushinda Bundesliga kwa mara ya nne mfululizo na kuiweka timu hiyo inayopewa mafunzo na kocha nyota Pep Guardiola ikiwa na pointi nane zaidi kuliko timu inayofuatia Borussia Dortmund.
Kocha wa Hamburg Bruno Labbadia amelalamika kwamba timu yake ilitoa zawadi ya ushindi kwa Bayern kwa kufungwa mabao ambayo hayakustahili. Labbadia amesema hakuna mabao ambayo yalitokana na mtiririko wa mchezo , lakini hii ni kitu cha kawaida kwa kuwa Bayern ina wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa.
Mchezaji wa kati wa Hamburg Aaron Hunt amekubali kwamba hakuna sababu ya kujiinamia na kuendelea kusikitika kutokana na mchezo huo.
"Ni wazi kwamba tunaweza kuishi na hali hiyo. Lakini kimsingi tumeambulia patupu, kwamba hatukuweza kushinda pambano hilo. Kwa hali hiyo tumesikitishwa, kwa kuwa tulifanya kazi mzuri sana. Bahati mbaya."
Licha ya kuwa ligi ya Ujerumani inaonekana kuwa ya upande mmoja na Bayern Munich na Borussia Dortmund zikionekana kutunisha misuli kwa kundi lote la timu za daraja la kwanza, lakini kuna mpambano mkali kati ya washambuliaji wawili wa timu hizo , Pierre-Emerick Aubameyang na Robert Lewandowski kuwania taji la mfungaji bora msimu huu.
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Poland ana mabao 17 baada ya michezo 18 ya ligi , lakini anaupungufu wa bao moja dhidi ya mpinzani wake Aubameyang ambaye ana mabao 18 katika michezo 18 ya Bundesliga.
Pointi 16 zinaitenganisha timu ya Bayern na timu iliyoko nafasi ya 3 Hertha Berlin na Dortmund iko katikati.
Aubameyanga alishindwa kuziona nyavu katika mchezo wa Jumamosi ambapo Borussia Dortmund iliishinda Borussia Moenchengladbach kwa mabao 3-1, ikiwa ni mchezo wa tano wa ligi msimu huu ambapo hakuziona nyavu, lakini ameweka mpira wavuni mara 27 katika mashindano yote msimu huu.
Alexander Meier alizifumania nyavu mara tatu jana Jumapili wakati Eintracht Frankfurt ikiibuka mshindi katika pambano lake na VFL Wolfsburg na kupata ushindi wa mabao 3-2.
Huu ni ushindi wa kwanza wa Eintracht Frankfurt nyumbani dhidi ya Wolfsburg tangu Novemba 2010.
Mlinzi wa kushito wa Frankfurt Bastian Oczipka amesema kwamba hali haikuwa nzuri kwa timu hiyo katika kipindi cha kwanza.
"Katika kipindi cha kwanza haikuwa rahisi kwetu. Mara baada ya kufungwa bao hali ya kujiamini ilitoweka kabisa. Tulipoteza mipira kila mara na ilikuwa tu bahati hatukufungwa zaidi. Katika kipindi cha pili tulisema, hatuwezi kuendelea kucheza vibaya. Tunapaswa kujitutumua na kupamabana na kurejea katika mchezo na sijui kama ilikuwa sahihi, lakini tulichokifanya kilikuwa barabara.
Schalke 04 nayo iliangukia pua pale ilipokandikwa mabao 3-1 na Werder Bremen jana Jumapili . Bremen bado iko katika nafasi ya 15 ikiwa sawa kwa pointi na VFB Stuttgart , ambapo Eintracht Frankfurt iko nafasi ya 14 ikiwa na pointi mbili zaidi.
Kocha wa Schalke Andre Breitenreiter amesema timu yake imepoteza nafasi nyingi za wazi.
"Inanibidi kujifinya kdogo , ili kutambua iwapo ni sawa yale niliyoyashuhudia hapa. Tulipata nafasi mara tatu za wazi ambazo hatukuzitumia. Tulicheza vizuri sana. Mambo mengi tuliyafanya vizuri , kila mtu aliona katika mchezo huo. Tulitengeneza nafasi nyingi za kupata mabao kuliko wakati mwingine wowote. Lakini bahati mbaya magoli ndio yanayohesabiwa katika mchezo, ili kuweza kushinda. Lakini kwetu haikuwa hivyo."
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / dpae / afpe
Mhariri: Yusuf Saumu