1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge Israel lapitisha sheria tata ya utaifa wa Kiyahudi

19 Julai 2018

Bunge la Israel limepitisha sheria inayoielezea Israel kama taifa huru la Wayahudi na kushusha hadhi ya lugha ya Kiarabu kutoka lugha rasmi na kuwa lugha yenye hadhi maalumu.

Israel Protest von arabischen Abgeordneten gegen US-Vizepräsident Pence in Knesset
Picha: Reuters/A. Schalit

Baadhi ya wabunge wa Kiarabu walipiga kelele na kuchanachana makaratasi baada ya kura hiyo, na kiongozi wa chama chao Yaman Odeh, amesema katika taarifa kuwa sheria hiyo inachokifanya ni kutoa hadhi ya kisheria kwa utengano na ubaguzi, na kuongeza kuwa hiyo ni sheria ya ubora wa Wayahudi inayowaweka kando zaidi ya asilimia 20 ya raia, ambayo imetengenezwa kukaidi, kugawa na kundeleza uchochezi wa serikali ya waziri mkuu Benjamin Netanyahu.

Serikali ya Israel inasema sheria hiyo  itaipa tu hadhi ya kisheria hali ya sasa ya Israel. Waziri Mkuu Netanyahu ametetea sheria hiyo na kusema kupitishwa kwake ni hatua muhimu katika kumbukumbu za vuguvugu la uzayuni na historia ya taifa la Israel.

"Tutaendelea kuhakikisha haki za kiraia katika demokrasia ya Israel, haki hizi hazitakiukwa, lakini pia walio wengi wana haki na walio wengi ndio wanaamua. Waliowengi zaidi wanataka kuhakikisha hadhi ya Kiyahudi ya taifa letu kwa vizazi vingi vijavyo," alisema Netanyahu baada ya kura hiyo.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.Picha: Getty Images/AFP/S. Scheiner

Sheria hiyo ambayo inatajwa kuwa ya kiishara zaidi, imepitishwa muda mchache baada ya nchi hiyo kuadhimisha miaka 70 tangu kuundwa kwa taifa la Israel. Inaainisha kwamba Israel ndiyo taifa la kihitoria la Wayahudi na wana haki ya kipekee ya uhuru katika taifa hilo.

Sheria ya ubaguzi na utengano

Pia sheria hiyo imeiondolea lugha ya Kirabu hadhi yake kama lugha rasmi sambamba na Kiebrania, na kuishusha kuwa "hadhi maalumu" inayoiwezesha kuendelea kutumika katika taasisi za nchini humo.

Waarabu wa Israel wanafikia milioni 1.8, sawa na karibu asilimia 20 ya idadi jumla ya wakaazi milioni 9. Rasimu za awali za sheria hiyo zilikwenda mbali katika kile wakosoaji ndani na nje waliona kama ubaguzi dhidi ya raia wa Kiarabu, ambalo kw amuda mrefu wamelalamika kuchukuliwa kama raia wa daraja la pili.

Vipengelee kadhaa vilivyoondolewa katika dakika za mwisho kufuatia upinzani wa rais wa Israel na mwanasheria mkuu, vingejumlisha kuanzishwa kwa jamii za Wayahudi pekee, na kuziangiza mahakama kuhukumu kwa mujibu wa sharia za Kiyahudi panapokuwa hakuna hukumu ya mfano katika suala husika.

Israel ilundwa mwaka 1948 kufuatia vita kati ya Wayahudi na Waarabu.Picha: picture-alliance/Zuma/N. Alon

Lakini hata baada ya mabadiliko, wakosoaji wamesemasheria hiyo mpya itaongeza hisia za kutengwa miongoni mwa jamii za Waarabu walio wachache.

"Muswada wa sheria ya utaifa ni uhalifu wa chuki, wanawabagua kabisaa raia wa Kiarabu, dhidi ya Waarabu wachache, ina ibara za kibaguzi, hasa zinazohusu makaazi ya Wayahudi, na zile zinazoshusha hadhi ya lugha ya Kiarabu," alisema Ahmed Tibi, mbunge wa chama cha Waarabu katika bunge la Knesset.

Jamii ya Waarabu wa Israel inahusisha hasa wazawa wa Wapalestina waliobakia kwenye ardhi yao waakti wa mgogoro kati ya Waarabu ya Wayahudi ambao ulisababisha vita vya mwaka 1948, vilivyopelekea kuundwa kwa taifa la sasa la Israel. Mamia kwa maelfu walilaazimika kuyaacha makaazi yao au kukimbia.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae,ape,ebu

Mhariri: Josephat Charo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW