1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge jipya la Serbia lapinga mpango wa Ahtisaari

Oummilkheir15 Februari 2007

Juhudi za kusaka maridhiano ya mzozo wa Kosovo zamwagiwa mxchanga na waserbia

Bunge la Serbia mjini Belgrade
Bunge la Serbia mjini BelgradePicha: AP Photo

Bunge jipya la Serbia lililokutana kwa mara ya kwanza jana baada ya uchaguzi mkuu wa mwezi uliopita,limepitisha kwa wingi mkubwa azimio linalolaani mpango wa Umoja wa mataifa unaoashiria aina fulani ya uhuru kwa jimbo la Kosovo.

Baada ya majadiliano marefu,waabunge 225 kati ya 244 waliohudhuria kikako hicho wameidhinisha azimio lililowasilishwa na serikali inayomaliza wadhifa wake na ambalo linalaani mapendekezo ya mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa Marti Ahtisaari kuhusu mustakbal wa Kosovo-jimbo linalosimamiwa na Umoja wa mataifa tangu mwaka 1999.

Wabunge 15 wamepinga azimio hilo na wane hawakuelemea upande wowote.

Azimio hilo linadhihirisha msingi wa msimamo wa serikali ya Belgrade katika mazungumzo ya February 21 ijayo pamoja na wakosovo wenye asili ya Albania mjini Vienna.

Msimamo huo mkali unatishia kukorofisha juhudi za kusaka maridhiano zinazoendeshwa na mjumbe maalum wa umoja wa mataifa Marti Ahtisaari.

Wakihutubia bunge mjini Belgrade,rais Boris Tadjic na waziri mkuu Vojislav Kostunica waliwataka hapo awali wabunge waupinge mpango huo wanaosema unavunja milki ya Serbia.Rais Boris Tadjic anasema:

“Kimsingi mpango huo si chochote isipokua kuiongoza Kosovo hadi uhuru.”

Rais Tadjic amesema Serbia itashiriki katika mazungumzo ya Vienna ili kutetea msimamo wake na kupendekeza mpango wake wenyewe ambao anautaja kua ni wa haki na unaoweza kukubalika..

Kwa upande wake waziri mkuu Vojislav Kostunica amesema Serbia iko tayari kuwapatia wakosovo wenye asili ya Albania mamlaka makubwa ya kujiamulia mambo yao na atakaeopinga anasema waziri mkuu, na hapa tunanukuu:” anataka kuimegua Serbia”-Mwisho wa kumnukuu waziri mkuu wa Serbia Vojislav Kostunica.

Mapema mwezi huu mjumbe maalum wa umoja wa mataifa Marti Ahtisaari alipendekeza aina ya mamlaka ya Kosovo itakayokua chini ya usimamizi wa kimataifa na kuongozwa na umoja wa Ulaya.

Kwa mujibu wa mapendekezo hayo,Kosovo inaweza kua mwanachama wa taasisi mbali mbali za kimataifa na kujivunia kanuni na vyenzo vya dola huru,ikiwa ni pamoja na katiba, bendera na wimbo wa taifa.

Pekee muungano wa upande wa upinzani cha kiliberali-LDP unaoongozwa na Cedomir Jovanovic ndicho kilichopinga azimio la serikali ya Serbia.

Jovanovic amesema azimio hilo ni mfululizo wa sera zilizoiangamiza Serbia.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW