1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Brazil lapinga mashtaka ya rushwa dhidi ya Temer

3 Agosti 2017

Bunge la Brazil limepiga kura kupinga mashtaka ya rushwa dhidi ya rais Michel Temer na hivyo kumuepusha kufikishwa mbele ya mahakama kuu, hatua ambayo ingesababisha aondolewe madarakani.

Brasilien Präsident Michel Temer in Brasilia
Picha: picture-alliance/dpa/PR/M. Correa

Wabunge wa Brazil wameyatupilia mbali mashtaka ya rushwa yaliyokuwa yanamkabili rais huyo anayeelemewa na kashfa na hivyo kumuepusha na kuwa rais wa pili wa Brazil kuondolewa madarakani katika kipindi cha mwaka mmoja. Licha ya kukabiliwa na madai mazito ya kupokea hongo, Temer alitarajiwa kuponyoka na kuendelea kuwa madarakani lakini jinsi alivyoponyoka kwa urahisi ni jambo la kushangaza wakati ambapo Brazil imo katika kampeni kubwa kabisa ya kupambana na rushwa.

Tawi la chini la bunge lilihitaji wingi wa theluthi mbili ya kura kuruhusu afunguliwe kesi kwenye mahakama kuu. Hata hivyo rais Temer alihitaji kupata thuluthi moja tu ya wabunge 172 ili kumuunga mkono au kutopiga kura ili mashtaka yaliyokuwa yanamkabili yatupiliwe mbali, Temer hatimaye aliungwa mkono na wabunge 263 kati ya 513. 

Rais huyo wa Brazil ameyaita matokeo hayo kuwa ni ushindi wa wazi amesema uamuzi uliopiitishwa na wabunge sio ushindi wa mtu binafsi lakini ni ushindi wa demokrasia katika nchi inayofuata utawala wa kisheria. Kiongozi huyo wa Brazil ameeleza kwamba kutokana na uamuzi huo ulio wazi sasa anaweza kusonga mbele katika kuchukua hatua za lazima ili kuitimiza kazi ambayo serikali yake iliianzisaha mwaka mmoja uliopita.      

Kuungwa mkono na wabunge kumemuongezea rais Temer matumaini ya kuweza kusonga mbele na hatua za kuleta mageuzi katika mfumo wa mafao ya wastaafu hatua ambayo ni muhimu katika kupunguza nakisi ya bajeti ya nchi hiyo na pia kurejesha imani ya wawekezaji. Uchumi wa Brazil umeanza kustawi tena baada ya kukabiliwa na mdororo.

Rais wa zamani wa Brazil Dilma RousseffPicha: Getty Images/AFP/Evaristo SA

Iwapo bunge la Brazil lingeruhusu kesi hiyo kupelekwa mahakama kuu rais Temer angelisimamishwa kazi kwa muda wa siku 180 na spika wa bunge angelikuwa rais wa kipindi cha mpito. Wapinzani wa mrengo wa kushoto, walitumai kwamba kashfa hio ingelimzamisha rais Temer na hivyo kuzuia mageuzi yake ya kiuchumi ya kubana matumizi yaliyo sababisha ghasia nchini Brazil. Wapinzani walitaka kulipiza kisasi  kutokana na rais Temer kuingia madarakani mwaka mmoja uliopita baada ya washirika wake bungeni kumtimua rais wa hapo awali Dilma Rousseff kwa kuvunja taratibu za bajeti.

Hata hivyo kunusurika kwa rais Temer kwa sasa sio mwisho wa mataitizo yake kwani bado inawezekana kwa mwendesha mashtaka mkuu nchini Brazil kumfungulia mashtaka mengine ya uhalifu. 

Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE/p.dw.com/p/2hYuD

Mhariri: Bruce Amani