1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la China lapitisha pendekezo la sheria ya usalama

28 Mei 2020

Bunge la China limeidhinisha mipango ya kutungwa sheria mpya ya usalama wa taifa mjini Hongkong katika hatua inayotarajiwa kuchochea ghasia katika kitovu hicho cha kibiashara na kuongeza mvutano kati yake na Marekani.

China Nationaler Volkskongress | Abstimmung Sicherheitsgesetz Hongkong
Picha: Reuters/C. G. Rawlins

Sheria hiyo inakiuka sheria za ndani za Hong Kong za kutoa adhabu kwa vitendo vinayoonekana kuhatarisha usalama wa kitaifa na kupindua nguvu ya serikali katika eneo hilo. China pia huenda ikaweka vitengo vya idara zake za kitaifa mjini Hong Kong kukabiliana na ghasia na kile kinachotajwa kuwa muingilio wa mataifa ya kigeni.

Zaidi ya wajumbe 2,800 wa Baraza la Taifa la Umma wa China wamepiga kura mwishoni mwa kikao cha  mwaka cha baraza hilo kuunga mkono pendekezo la kutungwa sheria hiyo huku mmoja akipinga pendekezo hilo na sita wakikosa kushiriki.

Kwa mujibu wa naibu msemaji wa serikali ya Ujerumani Ulrike Demmer, Ujerumani inaamini  ni muhimu kudumisha kiwango kikubwa cha uhuru ambao eneo hilo maalumu la uongozi linafurahia kwa sheria hii na hii na kwamba ndio njia ya pekee ya kudumisha uthabiti wa kijamii na maendeleo ya kiuchumi katika eneo la Hong Kong.

Carrie Lam- Kiongozi wa Hong KongPicha: Reuters/J. Silva

Katika wiki iliyopita, sheria hiyo iliibua ghadhabu mpya na maandamano katika eneo hilo lililokuwa koloni ya Uingereza ambapo watu wamekuwa wakifurahia kiasi cha uhuru ambao haujawahi kuonekana katika eneo la China bara.Wakosoaji na wanaharakati wa kutetea haki wanahofu kuwa sheria hiyo itatumika kukabiliana na tofauti za kisiasa. Sheria hiyo huenda ikabadilisha kwa kiasi kikubwa uhusiano kati ya Marekani na Hong Kong pamoja na serikali ya China

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo, amesema kuwa hadhi ya Hong Kong imeondolewa kwasababu serikali ya China haizingatii tena makubaliano yake na Uingereza ya kuiruhusu Hong Kong kuwa na kiwango cha juu cha uhuru. China ilitoa kipaombele kwa pendekezo hilo la sheria ya usalama wakati wa kikao cha Baraza la Taifa la Umma  baada ya maandamano makubwa ya kutetea demokrasia yaliokumba Hong Kong kwa takriban miezi saba mwaka jana.

Sheria hiyo itawaadhibu wanaojihusisha na kutaka kujitenga, kudhoofisha nguvu ya serikali,  ugaidi  na vitendo vyote vinavyotishia usalama wa taifa. Mbunge mmoja anaetetea demokrasia Claudia Mo, ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba, huu ndio mwisho wa Hong Kong na kwamba wanafahamu kuwa maadili ambayo wamekuwa wakizingatia kama vile haki za binadamu, uongozi wa sheria na kutetea demokrasia yameondolewa.

Mwanaharakati mmoja wa demokrasia Nathan Law pia ameliambi shirika hilo la AFP kwamba serikali inapaswa kuelewa kwanini watu wamekasirika  na kwamba chini ya muundo wa serikali moja na mifumo miwili uliokubaliwa kabla ya Hong Kong kurejeshwa kwa serikali ya China kutoka chini ya ukoloni wa Uingereza, Hong Kong inapaswa kuhakikihsiwa uhuru wa kiasi fulani ambao haupatikani China bara hadi mwaka 2047 .