1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Colombia laidhinisha makubaliano ya amani

Caro Robi
1 Desemba 2016

Bunge la Colombia limeidhinisha rasmi makubaliano ya amani kati ya Serikali na waasi wa kundi la FARC na hivyo kuashiria kuwa mzozo ambao umedumu kwa miaka hamsini nchini humo umefikia kikomo.

Kolumbien Bogota Unterzeichnung Friedensvertrag
Picha: picture-alliance/AP Photo/F. Vergara

Taarifa kutoka bunge zimesema makubaliano hayo yaliyofanyiwa mageuzi kadhaa yameidhinishwa kwa kura 130 kwa sufuri baada ya Baraza la seneti hapo jana pia kupiga kura kwa kauli moja kuyaidhinisha.

Rais wa Colombia Juan Manuel dos Santos ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel ya mwaka huu kutokana na juhudi zake za kutafuta amani nchini mwake, ameitaja kura hiyo ya bunge kama ridhaa muhimu kwa makubaliano ya amani ambayo amekuwa akiyatafuta.

Waasi kupokonywa silaha

Rais huyo amesema wapiganaji wa FARC wapatao 7,000 sharti waanze kuondoka kutoka ngome zao kuelekea maeneo yanayotajwa ya amani katika kipindi cha siku tano zijazo kuanzia leo na kuongeza shughuli ya kuwapokonya silaha itaanza katika kipindi cha siku thelathini zijazo.

Baraza la Seneti la ColombiaPicha: Getty Images/AFP/G. Legaria

Baada ya miaka 52 ya vita, zaidi ya miaka minne ya mazungumzo na sherehe mbili ya kutiwa saini makubaliano, kuridhia kwa mabunge yote mawili kwa makubaliano hayo ya amani kunawaruhusu waasi wa FARC kuweka chini silaha na kujiunga na siasa.

Makubaliano yalishindwa kufikiwa chini ya tawala za Marais waliopita Belisario Betancur aliyehudumu kati ya mwaka 1982-1986, Cesar Gaviria  aliyetawala 1990-1994 na Andres Pastrana aliyeingia madarakani 1998-2002.

Rais Santos na kiongozi wa FARC Rodrigo Londono walitia saini makubaliano yaliyofanyiwa marekebisho wiki iliyopita. Mnamo mwezi Oktoba, makubaliano yalishindwa kutekelezwa baada ya wapiga kura kuyapoinga katika kura ya maoni. Rais dos Santos amesema hakutakuwa na kura nyingine ya maoni.

Raia wa Colombia na wanasiasa wa upinzani walipinga vipengee vya makubaliano vinavyowaruhusu viongozi wa waasi kushikilia nyadhifa za uongozi serikalini na kutofungwa jela.

Santos asema hakutakuwa na kura ya maoni

Mpinzani mkubwa wa makubaliano hayo ya amani Rais wa zamani wa Colombia Alvaro Uribe ambaye sasa ni seneta na washirika wake wanadai makubaliano hayo yanawapa kinga waasi ambao wana hatia ya kufanya uhalifu wa kivita, kwa kuwapa viti bungeni badala ya kuwafunga jela.

Rais wa Colombia Juan Manuel Santos na kiongozi wa FARC Timoleon JimenezPicha: Getty Images/AFP/L. Robayo

Wabunge wa upinzani wa Baraza la Seneti na wa bunge la kawaida waliondoka kususia kura za kuyaidhinisha makubaliano hayo. Raia wanaoyapinga na kuyaunga mkono makubaliano hayo ya kihistoria waliandamana jana nje ya majengo ya bunge.

Mzozo huo wa Colombia umesababisha vifo vya zaidi ya watu 220,00, 60,000 hawajulikani waliko na kusababisha mamilioni ya watu kuyahama makazi yao. Serikali ya Colombia inakadiria kuwa mzozo huo wa muda mrefu zaidi katika kanda ya Amerika ya Kusini umewaathiri zaidi ya watu milioni 7.6.

Mwandishi: Caro Robi//Afp/Reuters/dpa

Mhariri:Josephat Charo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW