Bunge la Irak lalaani vikali shambulizi la Uturuki
17 Desemba 2007Bunge la Irak leo limelaani vikali shambulizi la angani lililofanywa na Uturuki dhidiy a ngome za waasi wa kikurdi kaskazini mwa Irak. Bunge hilo limeitaka Uturuki ishauriane na viongozi wa Irak kabla kuchukua hatua kama hiyo katika siku za usoni na isiwalenge Wairak.
Umoja wa Ulaya umeelezea wasiwasi wake hii leo kuhusu uvamizi huo na kuitaka serikali ya mjini Ankara ijizuie isifanye mashambulizi dhidi ya waasi wa chama cha PKK.
Ureno ambayo inashikilia urais wa umoja huo imeitaka Uturuki iheshimu mipaka ya Irak na ijizuie kufanya harakati za kijeshi zinazoweza kuvuruga amani na uthabiti wa eneo zima.
Mashambulizi ya mpakani dhidi ya ngome za waasi wa PKK yalisabisha kifo cha mtu mmoja na raia kadhaa wakajeruhiwa.
Marekani imekanusha madai kwamba iliamuru shambulizi la angani lakini maafisa wake wamekiri walijulishwa kabla harakati hiyo kufanywa. Jeshi la Uturuki lina wanajeshi takriban 100,000 karibu na mpaka wa Irak.