1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Israel lamchagua Rais mpya

10 Juni 2014

Bunge la Israel leo linamchagua rais wa kumi wa kuliongoza taifa hilo atakayechukua wadhifa huo kutoka kwa Shimon Peres ambaye muda wake wa kuhudumu unakamilika mwezi ujao

Picha: picture alliance/AP Photo

Bunge la Israel leo linamchagua rais wa kumi wa kuliongoza taifa hilo atakayechukua wadhifa huo kutoka kwa Shimon Peres ambaye muda wake wa kuhudumu unakamilika mwezi ujao.Caro Robi na taarifa kamili:

Wabunge wa 120 wa bunge la Israel lijulikanalo kama Knesser wanakutana leo kwa kikao maalum ambapo watamchagua kiongozi mpya wa nchi hiyo miongoni mwa wagombea watano wanaowania kiti hicho cha Rais.

Hakuna anayepigiwa upatu

Awali kulikuwa na wagombea sita,watatu kati yao wakiwa ni wabunge wa bunge la sasa lakini mmoja wao Binyamin Ben Eliezer wa chama cha Leba alijiondoa kutoka kinyang'anyiro hicho mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya polisi kuanzisha uchunguzi kuhusu madai ya ufisadi.

Mgombea urais wa Israel Reuven RivlinPicha: picture-alliance/dpa

Licha ya kuwa hakuna mgombea yeyote kati ya watano hao waliosalia anaepigiwa upatu kuibuka na ushindi,spika wa zamani wa bunge Reuven Rivlin ambaye ni mwanachama wa muda mrefu wa chama cha waziri mkuu Benjamin Netanyahu cha Likud anatajikana kuwa na uungwaji mkono mkubwa zaidi.Hata hivyo wachambuzi wanaonya kuwa huenda akachomoza mshindi ambaye hakutarajiwa.

Hakuna mgombea aliye na haiba inayolingana na Rais anayeondoka madarakani tarehe 27 mwezi Julai Shinmon Peres ambaye umaarufu na utashi wake ulimwezesha kuwa na usemi mkubwa katika wadhifa huo wa rais ambao kidesturi hauna madaraka ya kiutendaji na kuutumia kuhimiza ujumbe wa kisiasa unaopendelea kuwepo kwa amani.

Wagombea wengine mbali na Rivlin ni Meir Sheetrit wa chama cha mrengo wa kati cha Ha Tnuah, ni pamoja na Dalia Itzik ambaye mwaka 2006 alikuwa mwanamke wa kwanza kuwa spika wa bunge la Israel,Jaji mkuu mstaafu Dalia Dorner na mshindi wa tuzo ya Nobel ya kemia Dan Schectman.

Kutokana na ile hali kwamba hakuna mgombea anayetarajiwa kuapata kura 61 zinazohitajika kutangazwa mshindi,kuna uwezekano mkubwa kwa zoezi hilo kuingia katika duru ya pili leo alasiri na matokeo kamili yanatarajiwa kutangazwa jioni.

Wachambuzi wanakubaliana kuwa Rivlin atafuzu kwa duru ya pili lakini atakayepambana naye katika duru hiyo ya pili ya kura bado hajajulikana ila inadokezwa kuwa huenda ikawa ni Dorner au Itzik.

Schetman ambaye aliibuka katika nafasi ya pili kwa umaarufu kulingana na kura za maoni zilizochapishwa mwezi uliopita anaorodheshwa wa mwisho hivi sasa huku akikosa uungwaji mkono kutoka kwa wabunge.

Peres anaenziwa sana Israel

Peres ambaye ni miongoni mwa wa waanzilishi wa taifa la Israel,amekuwa katika hatamu za uongozi kwa miaka saba na amekuwa mkakamavu katika majukumu yake licha ya umri mkubwa huku akitimiza miaka 91 mwezi ujao.

Shimon Peres na Mahmud AbbasPicha: picture-alliance/dpa

Peres ni maarufu sana miongoni mwa waisrael wengi huku thuluthi mbili ya raia hao walikuwa wanataka asalie kuwa rais wao.Kuondoka kwake madarakani kutaelekeza darubini sasa kutoka masuala ya kimataifa na kuangazia zaidi masuala ya ndani ya Israel.

Wagombea wote watano wa urais wameahidi kuheshimu wajibu na mamlaka ya wadhifa huo na kuliunganisha taifa.Peres na waziri mkuu Benjamin Netanyahu walitofautiana kuhusiana na mzozo kati ya Israel na Palestina na pia mshindi huyo wa tuzo ya amani ya Nobel alizungumzia wazi suala la mahusiano na Marekani na Iran kuhusu mpango wake wa kinyuklia.

Wengi watamkumbuka kiongozi huyo kwa kurejesha hadhi ya wadhifa huo wa rais nchini Israel ambao ulitiwa doa kubwa na mtangulizi wake Moshe Katsav ambaye alishitakiwa kwa makosa ya ubakaji na udhalilishaji wa kingono.

Mwandishi:Caro Robi/afp

Mhariri:Hamidou Oummilkheir