Bunge la Israeli sasa kuchagua waziri mkuu.
16 Aprili 2020Rais Reuven Rivlin alichukua hatua hiyo baada ya waziri mkuu wake mteule na mkuu wa zamani wa jeshi Benny Gantz, pamoja na waziri mkuu Benjamin Netanyahu kushindwa kufikia makubaliano ya kugawana madaraka wakati muda wa mwisho ukifikia ukingoni usiku wa manane kuamkia leo.
Wapinzani hao wakubwa waliahidi kuunda serikali ya dharura itakayoongoza taifa katikati ya mzozo wa virusi vya corona, uliovuruga uchumi na kusababisha kiwango cha ukosefu wa ajira kuongezeka sana. lakini baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa wiki kadhaa na kushindwa kuzaa matunda, ikiwa ni pamoja na masaa 48 ya mwisho yaliyoongezwa na rais Rivlin, hatimaye amekiri kupoteza imani na fursa ya kufikiwa kwa makubaliano.
Rais Rivlin alinukuliwa akiwaambia wabunge kwamba ana imani wataweza kupata wingi utakaofanikisha kuundwa serikali mapema iwezekanavyo ili kuzuia duru ya nne uchaguzi.
Uamuzi wa rais Rivlin anayesimamia mazungumzo ya baada ya uchaguzi kwa lengo la kuunda serikali, hauondoi uwezekano wa kufanyika makubaliano kati ya Netanyahu na Gantz. Baada ya muda wa mwisho kupita, chama cha Likud cha Netanyahu na chama cha Bluu na Nyeupe cha Gantz vimesema huenda wataendeleza majadiliano baina yao hii leo. Netanyahu pia alisema alimualika Gantz kwenye mkutano mwingine leo jioni.
Hivi sasa wamesaliwa na wiki tatu za mwisho za kukamilisha makubaliano. Vinginevyo, bunge linaweza kuvunjwa na kwa mara nyingine taifa hilo litaingia kwenye uchaguzi. Lakini hata hivyo, Netanyahu anaonekana kupata nguvu, hasa baada ya Gantz kushindwa kutumia fursa yake ya kuunda serikali.
Ni jumla ya wabunge 59 waliomuidhinisha Netanyahu, na kumuacha akiwa amepungukiwa viti vichache tu vya wingi unaostahili bunge lenye viti 120. Wakati akiendelea kuzungumza na Gantz, anaweza kujaribu kuwashawishi wabunge wawili kutoka upinzani kwa matumaini ya kuunda serikali ya wingi mdogo.
Bunge linaweza kuchagua mgombea wa watu kuwa waziri mkuu, lakini haionekani kama kuna mbadala anayefaa na anayeweza kuungwa mkono na wabunge 61.
Netanyahu na Gantz walieonekana kukaribia kufikia makubaliano wiki iliyopita. Lakini makubaliano hayo yalisimama, na ikiripotiwa ilisababishwa na masharti ya Netanyahu ya kuwa na ushawishi zaidi kwenye uteuzi wa mahakama. Ikumbukwe Netanyahu anakabiliwa na kesi ya ufisadi, kuvunja imani na ubadhirifu, ingawa anayakana madai hayo.
Uchunguzi wa maoni uliochapishwa Jumatatu nchini humo ulionyesha chama cha Likud kikijiongezea uungwaji mkono, hatua itakayomwezesha Netanyahu kushinda uchaguzi.
Soma Zaidi: Uchaguzi wa Israel: Netanyahu vs Gantz duru ya 3
Mashirika: APE/RTRE