Bunge la Kenya kuwahoji wateule wa uwaziri
12 Oktoba 2022Kamati hiyo inasubiriwa kuwasilisha ripoti yake bungeni katika muda wa siku 28. Wakati huohuo, baadhi ya mawaziri walioteuliwa waliokuwa wakiandamwa na kesi za ufisadi wamefutiwa mashtaka.
Kwenye mjadala uliowasilishwa na mwakilishi wa chama tawala Kimani Ichungwa, bunge la taifa limeyaridhia majina ya wanachama 21 wa kamati ya uteuzi waliochaguliwa na kamati ya operesheni za bunge. Kamati hiyo ya uteuzi sasa inawajibika kuanza mchakato wa kuwapiga msasa mawaziri wapya walioteuliwa na kuwasilisha ripoti yake bungeni ifikapo tarehe 27 mwezi huu wa Oktoba.
Upinzani wa Kenya, Azimio la Umoja One Kenya umejipangwa kwa maswali magumu
Kwa upande wao wabunge wa upinzani wa Azimio la Umoja One Kenya wanashikilia kuwa watawauliza mawaziri hao wapya maswali magumu hasa kuhusu suala la uadilifu kwa baadhi.Kauli hizo zinaungwa mkono na kiongozi wa chama cha Wiper Demokratik Kalonzo Musyoka anayehisi kuwa Rais Ruto alikuwa anaosha mikono yake alipoyataja baadhi ya majina.
Mwakilishi wa upizani bungeni Opiyo Wandayi aliyepia mbunge wa Ugunja alisisitiza kuwa watalikagua baraza hilo jipya kuhakikisha kuwa linatimiza vigezo vya jinsia, uwakilishi wa maeneo, kabila na walio na ulemavu.
Soma zaidi:Upinzani wamkosoa Ruto kwa kwa kuruhusu vyakula vilivyokuzwa kisayansi
Kamati ya uteuzi inawaleta pamoja wabunge wa Kenya Kwanza na azimio la Umoja One Kenya.Ifahamike kuwa Kenya kwanza ndiyo iliyo na wingi wa uwakilishi bungeni na hilo linaaminika kuwa litaipisha shughuli ya kuwapiga msasa mawaziri wapya bila pingamizi au vikwazo.
Yote hayo yakiendelea,mwendesha mashtaka mkuu, DPP Nurdin Haji, amefutilia mbali mashtaka yanayomuandama Aisha Jumwa aliyeteuliwa kuwa waziri wa jinsia na huduma za umma.Kufuatia hilo,seneta wa Narok Ledama Ole Kina kupitia mtandao wa Twitter, amekitaja kitendo hicho kuwa cha kuwatakasa walioteuliwa ili kuwahalalisha.
Mwendesha mashtaka mkuu hii leo alifutilia mbali amshtaka ya ufisadi yaliyomundama mbunge wa zamani wa Malindi Aisha Jumwa kwa kufuja shilingi milioni 19 za hazina ya maeneo bunge.
Waziri mteule ameshtakiwa kwa matumizi ya mabaya ya madaraka
Wakati huohuo, seneta wa Meru wa zamani, Mithika Linturi aliyeteuliwa kuwa waziri wa kilimo ameshtakiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka.Waziri mteule wa fedha, Profesa Njuguna Ndung'u anaandamwa na tuhuma za ufisadi alipokuwa gavana wa benki kuu ya Kenya baada ya zaidi ya shilingi bilioni 2 kupotea wakati kandarasi ya kuchapisha hela ya De La Rue kusitishwa.
Kamati ya uteuzi ina muda wa siku 28 kuwasilisha ripoti ya mawaziri hao wapya bungeni kabla ya kujadiliwa na kupata ridhaa ya rais.Bunge la taifa lina muda hadi tarehe 3 Novemba kuitoa ridhaa yake.
DW Nairobi