1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Kenya lapokea hoja ya kumuondosha makamu wa rais

1 Oktoba 2024

Wabunge nchini Kenya wameanzisha mchakato wa kumtimua Makamu wa Rais Rigathi Gachagua, baada ya kuwasilisha hoja yenye makosa 10 yakiwemo ya ufisadi, kumdharau rais na kuendekeza ukabila.

Makamu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua.
Makamu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua.Picha: LUIS TATO /AFP via Getty Images

Muda mfupi kabla saa 9:00, Spika wa Bunge la Taifa, Moses Wetangula, alifungua kikao ili kuupisha mjadala wa kumtimua Naibu Rais Rigathi Gachagua.

ikao kilijaa pomoni na wabunge walishangilia kwa kupiga miguu chini wakati hoja hiyo ilipowasilishwa.

Gachagua analaumiwa kwa kumdhihaki Rais William Ruto, kueneza ukabila, kujilimbikizia mali kwa njia za ufisadi na kutumia vibaya madaraka.

Soma zaidi: Bunge la Kenya lapokea hoja ya kuuzuliwa makamu wa rais

Kimsingi, hoja hiyo imesema makamu huyo wa rais amekiuka Ibara ya 10 na 27 ya katiba "kwa kuendekeza ukabila na upendeleo wa waziwazi pamoja na kutumia vibaya afisi yake. 

Wabunge hao walijawa na bashasha pale majina yao yalipotajwa kuthibitisha kuwa waliridhia saini zao kuorodheshwa kwenye hoja iliyowasilishwa na Mwengi Mutuse, mbunge wa Kibwezi Magharibi na Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria ya Bunge (JLAC).

Wabunge 291 waidhinisha hoja kuwasilishwa

Jumla ya wabunge 291 walitia saini hoja hiyo ya kumtimua makamu wa rais wa Kenya.

Millie Odhiambo, kiranja wa upinzani na mbunge wa Suba North, alisisitiza kuwa siasa za kulipiza kisasi zimepitwa na wakati.

Rais William Ruto wa Kenya.Picha: Bianca Otero/ZUMA Press Wire/IMAGO IMAGES

Soma zaidi: Amenya asema maisha yako hatarini

"Mlisema tusiuguse Mlima. Lakini kama umemgusa Raila, sisi tunaugusa Mlima. Nimetia saini. Na tumenyamaza. Ukiona tumenyamaza, usidhani tumebadilika…..bado sisi ni wale wale!”

Mara ya mwisho kwa makamu wa rais wa Kenya kujikuta kwenye hali kama hii ni mwaka 1989 pale Dk. Josephat Karanja alipopigiwa kura ya kutokuwa na imani naye kwa kumdharau rais wa wakati huo, Daniel arap Moi, na akajiuzulu.

Hadi ripoti hii inatayarishwa, bunge lilikuwa linasubiria muongozo kutoka kwa Spika Wetangula.

Pendekezo la kutokuwa na imani na Rais Ruto

Rais William Ruto wa Kenya (kushoto) na makamu wake, Rigathi Gachagua.Picha: Simon Maina/AFP

Katika kile kinachoonesha kulipiza kisasi, Seneta Dan Maanzo wa Makueni naye aliwasilisha pendekezo la kutokuwa na imani na Rais Ruto kwa "kushindwa kuwalinda Wakenya kama kiongozi wa taifa na kushindwa kuyafanyia kazi masuala yanayowatatiza Wakenya."

Soma zaidi: Amnesty yataka tume kuundwa kuchunguza vifo vya waandamanaji Kenya

Pendekezo la kutomuamini kiongozi linatoa nafasi ya kuwasilisha maoni mazito yanayowatuhumu viongozi ambayo yanaweza kufanyiwa mjadala na kupitishwa na kura ya wengi.

Bado haijawa wazi ikiwa hoja ya Maanzo itaweza kupata wingi wa kutosha kuweza kukubalika kujadiliwa bungeni.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW