1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Kongo laidhinisha serikali ya Waziri Mkuu Suminwa

Jean Noël Ba-Mweze
12 Juni 2024

Wabunge nchini Kongo Jumatano 12.06.2024 kuidhinisha mpango wa utekelezaji wa serikali ya Waziri Mkuu Judith Suminwa uliokuwa ukingojewa kwa hamu.

Wabunge 398 miongoni mwa 405 walipiga kura ya ndio kuidhiniha serikali mpya nchini Kongo
Wabunge 398 miongoni mwa 405 walipiga kura ya ndio kuidhiniha serikali mpya nchini KongoPicha: Getty Images/AFP/J.D. Kannah

Wabunge waliidhinisha kwa uwingi mpango huo wa utekelezaji ambao vipaumbele vyake vimekusanywa katika nguzo sita.

Nazo ni kujenga uchumi ili kuunda kazi na kulinda uwezo wa ununuzi, kulinda mamlaka ya kitaifa na usalama wa raia pamoja na mali zao, kuhakikisha upatikanaji wa huduma za msingi za kijamii, kuimarisha uwezo wa Wakongo kushiriki katika ujenzi wa nchi, kusimamia ipasavyo mfumo wa ikolojia ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Waziri Mkuu, Judith Suminwa, anaamini fedha hizo zitaruhusu kutekeleza mpango huo:

"Mpango wa utekelezaji wa serikali utahudumiwa kifedha na serikali ya kitaifa, zile za mikoa pamoja na majimbo. Asilimia 30 ya fedha za mpango huu itasaidia kuunda kazi na kulinda uwezo wa ununuzi. Asilimia 25 itasaidia kwa kulinda eneo la kitaifa.", alisema Suminwa.

Kuboreshwa kwa kilimo nchini Kongo

Wabunge wa kitaifa walitoa mapendekezo mbalimbali ili serikali kuimarisha mpango wake. Vital Kamerhe, ambaye ni Spika wa Bunge, alisisitiza kuimarisha kilimo nchini Kongo. 

"Je, haiwezikani kuuomba kila mkoa kulima hekta kadhaa? Fedha hizo zinapotoka ndani ya benki kwa kilimo kutakuwa na ukosefu wa fedha. Lakini tunapovuna tutapata fedha kwa uwingi na fedha zetu zitakuwa tena na thamani. Ndiyo siri ya Brazil. Tuifanye hapa kwetu.", alisisitiza Kamerhe.

Upinzani wakosoa kile unachoita ''mpango hewa wa serikali''

Waziri Mkuu Judith Suminwa na rais Felix TshisekediPicha: DRC Presidency/Xinhua News Agency/picture alliance

Kwa upande wake, upinzani unaamini kuwa mpango huo ni bure tu na kiasi cha bilioni 93 kimetajwa tu ili kuwadanganya watu.

Ndivyo alivyoeleza Ferdinand Kambere, naibu katibu mkuu wa PPRD, chama cha rais wa zamani, Joseph Kabila. 

"Nchi inaendelea kuvamiwa na majeshi ya kigeni na kuna yale yaliyoalikwa na serikali yenyewe. Watu wanaendelea kuuawa.'', alisikitishwa Kambere.

Kabla ya kuhoji : ''Mabadiliko gani wanayotayarisha ili kuboresha hali? Yataanza vipi na kutekelezwa na serikali gani? Wakubali tu kwamba nchi ipo katika hali mahututi na kampeni yao ilikuwa ya kuwadanganya watu tu."

Hatimaye Kongo sasa tayari inakuwa na serikali rasmi. Serikali hiyo ambayo imetawazwa Jumatatu inaanza kazi karibu miezi sita baada ya Rais Félix Tshisekedi kuapishwa kwa muhula wa pili na zaidi ya miezi miwili baada ya kuteuliwa kwa Judith Suminwa kama Waziri Mkuu.