Bunge la kwanza la kihistoria laanza Myanmar
1 Februari 2016Chama cha National League for Democracy kilipata ushindi mkubwa katika uchaguzi uliofanyika Nov. 8, kikipata asilimia 80 ya viti katika bunge hilo dhidi ya chama cha Union Solidarity and Development Party kinachoungwa mkono na jeshi la nchi hiyo.
Wabunge kutoka vyama vyote viwili na kutoka katika upande wa vyama vinavyowakilisha wachache pamoja na wabunge wanaowakilisha upande wa jeshi walianza kwa hatua ya kula kiapo cha utii katika bunge hilo.
Hatua hii inafungua ukurasa mpya wa kihistoria katika siasa za nchi hiyo baada ya utawala wa kijeshi wa muda mrefu wa ukandamizaji lililotwaa madaraka ya uongozi wa taifa hilo tangu mwaka 1962. Mmoja wa wabunge wa bunge hilo ambaye ni mwakilishi wa jimbo la Yangon kwa tiketi ya NLD alisikika akisema.
Kiongozi wa chama cha NLD, Suu Kyi na wanasiasa wengine waliokuwa wakipigania kuwepo kwa utawala wa kidemokrasia nchini humo walifungwa jela huku shughuli za kisiasa zikipigwa marufuku.
Taifa hilo la kusini mashariki mwa bara la Asia lilianza harakati za kujinasua kutoka katika utawala wa kiimla kuelekea demokrasia mnamo mwaka 2011 wakati utawala huo wa kijeshi ulipokubali kukabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia iliyokuwa ikiongozwa na Jenerali Thein Sein ambaye tayari alikwisha kuwa mwanamageuzi.
Kiongozi huyo anatarajiwa kuachia madaraka hayo rasmi mwezi Machi au Aprili mwaka huu wakati kiongozi wa chama cha NLD atakapotwaa rasimi madaraka hayo ya Rais.
Katiba yambana Suu Kyi kuwa Rais.
Hata hivyo kiongozi wa chama cha NLD Suu Kyi anabanwa na katiba ya nchi hiyo kushika madaraka ya urais wa nchi hiyo na hadi sasa hajataja jina la atakayependekezwa na chama chake kushika madaraka hayo.
Licha ya ushindi huo mkubwa ambao chama cha NLD kilipata katika uchaguzi uliopita bado kinalazimika kugawana madaraka na jeshi na tayari Suu Kyi ameshakutana na viongozi waandamizi wa jeshi nchini humo ili kuhakikisha kuwa mabadiliko ya madaraka ya nchi hiyo yanafanyika katika njia salama na jeshi limeahidi kutoingilia utawala uliochaguliwa katika njia ya kidemokrasia.
Chama cha Thein Sein kilichokuwa kikiungwa mkono na jeshi kilishinda uchaguzi wa mwaka 2010 ambao chama cha NLD hakikushiriki kikidai kuwa mchakato wa uchaguzi huo haukufanyika katika mazingira ya haki na yenye usawa na baada ya mabadiliko kadhaa katika sheria ya uchaguzi nchini humo chama cha NLD kilifanikiwa kushinda chaguzi ndogo zilizofanyika nchini humo mwaka 2012.
Mwandishi: Isaac Gamba/ APE/ DPAE.
Mhariri: Iddi Ssessanga