Bunge la Lebanon lakosolewa kushindwa kuchagua rais
18 Juni 2023Kiongozi wa kidini wa kanisa la Meronite nchini Lebanon ameiita hatua ya bunge kushindwa kumchagua rais siku ya Jumatano kuwa ni ukiukwaji uliopangwa na mbaya kabisa wa katiba.
Kiongozi huyo Bechara Boutros al-Rai alisema kikao hicho cha bunge kilikuwa ni kama mchezo wa kuigiza, huku akimtolea mwito kila afisa kukiri makosa yake na kujirekebisha, kufuatia miezi minane ya ombwe la kimamlaka nchini humo.
Miaka minne tangu Lebanon ilipotumbukia kwenye mdororo wa kiuchumi, inaashiria mgogoro mbaya zaidi tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vya kati ya 1975-90.
Bunge la Lebanon siku ya Jumatano lilishindwa kwa mara ya 12 kumchagua mtu wa kujaza nafasi hiyo, ambayo chini ya mfumo wa kimadhehebu nchini humo, imetengwa kwa ajili ya Wakristu wa Maronite.