1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Libya lashindwa kuidhinisha tarehe ya uchaguzi

Angela Mdungu
28 Desemba 2021

Bunge la Libya jana lilishindwa kuidhinisha tarehe mpya ya kufanyika uchaguzi wa rais ulioahirishwa wiki iliyopita. Uchaguzi huo ulitazamwa kuwa njia ya kwanza kuelekea kupatikana amani nchini humo

Libyen | Parlament in Sirte
Picha: AA/picture alliance

Maamuzi hayo yalifanyika baada ya kumalizika kwa kikao kilichokuwa kimegubikwa na malumbano kilicholenga kuakisi mgogoro wa kisiasa unaohusu hatma ya mchakato wa amani nchini humo.

Uchaguzi wa Libya ulikusudiwa kufanyika Ijumaa iliyopita kama sehemu ya juhudi za kutaka kumaliza mzozo na machafuko yaliyodumu kwa muongo mmoja, kwa kumchagua rais na wabunge lakini uliahirishwa baada ya kuwepo kwa msuguano kuhusu kanuni zinazopaswa kutumika.

Wagombea, vyama vya kisiasa na wanasiasa tangu wakati huo wamekuwa wakilumbana juu ya muda gani uchaguzi huo unapaswa kuahirishwa na iwapo serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa ya waziri mkuu Abdulhamid al-Dbeibah inaweza kuendelea kuwa madarakani katika kipindi hiki.

Kikao cha bunge cha jana Jumatatu kilikuwa ndicho kikubwa zaidi tangu serikali ya Dbeibah ilipoingia madarakani mwezi Machi mwaka huu, na cha kwanza kuwakusanya wabunge wote kutoka katika pande zenye mgawanyiko zinazohasimiana.

Bila kushughulikia changamoto, uchaguzi hautaweza kufanyika

Wiki iliyopita, tume ya uchaguzi ya Libya ilisema, uchaguzi uliopangwa usingeweza kufanyika kutokana na kile ilichokiita mapungufu katika sheria ya uchaguzi na mchakato wa kukata rufaa, hivyo ilipendekeza kuusogeza mbele uchaguzi huo hadi Januari 24

Kamati ya bunge inayoshughulikia masuala ya chaguzi, ilitoa ripoti kuwa iwapo changamoto hazitoshughulikiwa, haitowezekana kufanya uchaguzi hata katika tarehe iliyotajwa. Kikao cha bunge cha jana kilichorushwa na televisheni kilivunjika baada ya kuzuka kwa malumbano na kinatarajiwa kuendelea leo Jumanne ili kupiga kura kuhusu mapendekezo kadhaa ikiwemo kucheleweshwa kwa uchaguzi.

Waziri mkuu wa Libya Abdul Hamid Mohammed DbeibahPicha: Hazem Ahmed/AP Photo/picture alliance

Kikao hicho kinatarajiwa pia kuzungumzia hatma serikali ya umoja wa kitaifa na uongozi wake chini ya waziri mkuu Dbeibah. Uhusika wa Dbeibah kama mgombea wa urais umekuwa sababu mojawapo kubwa ya mzozo kuhusu uchaguzi, wakati ripoti ya kamati ya bunge ya uchaguzi ikitoa wito wa kubadilisha serikali.

Baadhi ya watu wanatoa hoja kuwa, Waziri mkuu huyo wa Libya hakupaswa kuruhusiwa kuwa mgombea wa Urais kwakuwa aliahidi kutokufanya hivyo alipoingia madarakani. Mshauri maalumu wa Umoja wa Mataifa Stephanie Wiliams alisema jana Jumatatu kuwa kwa sasa kinachopaswa kuzingatiwa ni uchaguzi mkuu na siyo hatma ya serikali ya umoja wa kitaifa.

Wiki iliyopita, mataifa ya Magharibi yalisema yanaitambua serikali hiyo kuwa ni halali hadi pale itakapoabidhi madaraka kwa serikali mpya  baada ya uchaguzi. Hata hivyo mataifa hayo hayakuzungumzia lolote kuhusu  nafasi ya Dbeibah kama waziri mkuu.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW