1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Bunge la Marekani lagawika kuipa msaada Israel na Ukraine

Josephat Charo
2 Novemba 2023

Rais Joe Biden wa Marekani amelitaka bunge kwa haraka lipitishe msaada mpya kwa Israel na Ukraine wa thamani ya mabilioni ya dola. Baraza la wawakilishi linajiandaa kuupigia kura muswada wa sheria utakaoibana Ukraine.

USA Präsident Joe Biden
Rais wa Marekani, Joe BidenPicha: Ting Shen/Pool/abacca/picture alliance

Mjadala kuhusu maombi ya ufadhili kwa Ukraine na Israel unaanza kwa dhati leo kufuatia wiki kadhaa wakati wabunge wa chama cha Republican walipokuwa wakivutana kumchagua spika mpya, na haifahamiki wazi ikiwa kuna makubaliano yoyote yanayoweza kupitishwa na baraza la wawakilishi na baraza la seneti.

Wabunge wa chama cha Democratic na chama cha Republican wanataka kwa haraka kupitisha msaada wa kijeshi kwa Israel, mshirika wa muda mrefu wa Marekani ambaye yuko vitani na kundi la Hamas, linalotambulika kama la kigaidi nchini Ujerumani, Marekani na Umoja wa Ulaya. Hata hivyo mambo yanakuwa magumu zaidi linalopokuja suala la msaada kwa ajili ya Ukraine. Marekani ni mchangiaji mkubwa wa msaada wa kijeshi kwa Ukraine, baada ya kuipatia mabilioni ya dola serikali ya mjini Kiev tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mnamo Februari 2022.

Mbunge wa chama cha Democratic, na kiongozi wa walio wachache bungeni, Hakeem Jeffries anasema, "Nimekuwa wazi kabisa kwamba rais Biden amewasilisha muswada wa fedha unaojumuisha vipaumbele vya usalama wa taifa kwa Wamarekani, kuhusu kuisaidia Israel, kuisaidia Ukraine, kuwasaidia washirika wetu aktika eneo la Indo-Pasifiki. Kuhakikisha kwamba msaada wa kibinadamu kwa Wapalestina, raia wanaokabiliwa na hatari na kote ulimwenguni. Na naamini muswada huu unatakiwa uzingatiwe kwa ujumla wake"

Ahadi ya Biden kuisaidia Ukraine iko hatarini

Lakini ahadi ya rais Biden kuendelea kuisaidia kifedha Ukraine, iliyosisitizwa na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky wakati wa ziara yake mjini Washington mnamo mwezi Septemba, inaonekana kuwa hatarini. Katika baraza la wawakilishi ambako wabunge wa chama cha Republican ni wengi kidogo kuliko wale wa chama cha Democratic, baadhi ya wabunge mahafidhina wametaka ufadhili wa kifedha kwa ajili ya Ukraine ukome mara moja. Baraza la wawakilishi limejinasua kutokana na mkwamo wa wiki tatu baada ya spika wa zamani Kevin McCarthy kuondolewa kwa kura za kundi la wabunge hao mahafidhina.

Spika wa bunge la Marekani, Mike JohnsonPicha: Alex Brandon/AP Photo/picture alliance

Hali ni tofauti kabisa katika baraza la seneti linalodhibitiwa na chama cha Democratic, ambako wabunge wa chama cha Republican wameelezea kuunga mkono kuimarisha msaada kwa Ukraine. Seneta wa chama cha Republican Mitch McConnell alisema siku chache zilizopita kuwa wazo kwamba kuunga mkono vita dhidi ya uchokozi wa Urusi ni kutatiza na kuvuruga masuala mengine ya kipaumbele kiusalama si sahihi.

Akifahamu kwamba hali ya kuchoka kutokana na vita inazidi kuongezeka katika medani za siasa nchini Marekani, rais Biden ameamua kuunganisha pamoja maombi yake ya msaada kwa ajili ya Ukraine - zaidi ya dola bilioni 61, pamoja na msaada kwa Israel wa takriban dola bilioni 14.

Biden pia ameomba kiasi dola bilioni tisa kushughulikia mizozo ya kibinadamu, ikiwemo katika Ukanda wa Gaza, huku akijaribu kuufanya mswada ukubalike na mahafidhina kwa kuomba pia mabilioni ya dola kwa ajili ya usalama katika mpaka wa Marekani na miradi inayonuiwa kuikabili China. Kwa jumla fedha zinazoombwa katika muswada huo ni dola bilioni 106.

Wabunge wa baraza la wawakilishi, ambao hawajaridhishwa na kiwango anachokitaka rais Biden na ambao pia wamegawika kuhusu suala la Ukraine, hivi leo wanapanga kuupiga kura muswada kuhusu Israel pekee. Spika mpya Mike Johnson amesema na hapa tunanukuu "Hatuwezi kuturuhusu ukatili na uovu usio mithili unaoendelea sasa dhidi ya Israel uendelee." Spika huyo anataka hatua za kuwasaidia washirika wengine wa Marekani zinajadiliwe baadaye.

afpe

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW