1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge Marekani lapitisha mashtaka ya Trump mara ya pili

14 Januari 2021

Rais wa Marekani Donald Trump amekuwa rais wa kwanza wa Marekani ambaye mashtaka dhidi yake ya kutaka avuliwe madaraka yamepitishwa mara mbili kwa njia ya kura na baraza la wawakilishi wa nchi hiyo.

USA | Nancy Pelosi hält den Artikel der Amtsenthebung gegen Präsident Donald Trump
Picha: Alex Brandon/AP Photo/picture alliance

Wabunge wamemshutumu Trump kwa kuchochea vurugu kufuatia uvamizi wa majengo ya bunge wiki iliyopita.

Wabunge waliounga mkono mashtaka dhidi ya Trump wamesema alihusika kwa kuwachochea wafuasi wake kuvamia majengo ya bunge Capitol Hill mjini Washington.

Kura ya kutaka aondolewe uongoziniilipitishwa na wabunge 232 dhidi ya 197. Trump amekuwa rais wa kwanza wa Marekani ambaye mashtaka dhidi yake yamepitishwa mara mbili.

Wabunge 10 wa chama cha Republic waliungana na Wademocrat wakisema Rais Trump anapaswa kuwajibishwa, huku wakionya kuhusu kitisho cha dhahiri ikiwa bunge litamuacha bila kumwajibisha kabla ya Joe Biden kuchukua usukani.

Zikiwa zimesalia siku saba tu kabla ya muda wa Trump madarakani kumalizika, Wademocrat waliharakisha mchakato wa kutaka kumvua madarakani lakini makamu wa rais Mike Pence alikataa kuitikia miito ya kutumia ibara ya 25 ya katiba ya nchi hiyo kumuondoa ofisini.

Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Donald J. Trump via Twitter/REUTERS

Pelosi: Hakuna aliye juu ya sheria

Punde tu baada ya kura hiyo, spika wa bunge Nancy Pelosi alisema hatua hiyo ya baraza la wawakilishi inathibitisha kuwa hakuna yeyote aliye juu ya sheria.

"Leo kwa pande zote mbili, bunge limedhihirisha kwamba hakuna aliye juu ya sheria, hata rais wa Marekani. Na kwamba ni wazi kuwa Donald Trump ni kitisho cha sasa kwa taifa letu na kwa mara nyingine tumetekeleza wajibu wetu kwa kulinda katiba ya Marekani. Na sasa kwa masikitiko ya yale haya yanamaanisha kwa nchi yetu kuhusu rais atakayechochea uasi atasaini kukamatwa kwa kifungu cha mashtaka." Amesema Pelosi.

Trump ni kati ya marais watatu wa chama cha Republic ambao baraza la wawakilishi limepitisha mashtaka dhidi yao, lakini huenda akawa wa kwanza kushtakiwa katika baraza la senate baada ya kuondoka ofisini.Soma pia Trump asema hatahudhuria kuapishwa kwa Biden

Spika wa baraza la wawakilishi akiongoza mjadala wakati wa mashtaka ya kutaka kumuondoa Trump ofisiniPicha: J. Scott Applewhite/AP Photo/picture alliance

Mara ya kwanza ambapo mashtaka ya kutaka Trump avuliwe madaraka yalipitishwa na baraza la wawakilishi ni Disemba 2019, kuhusiana na shinikizo lake kwa Ukraine. Hata hivyo baraza la seneti lilipiga kura kumuondolea lawama.

Mashtaka kwa rais asiyekuwa madarakani. Je yawezekana?

Ingawa baadhi ya wasomi wa kisheria wanahoji kuwa rais wa zamani hawezi akashtakiwa katika baraza la seneti, baadhi ya maseneta wa zamani pamoja na majaji wamewahi kushtakiwa katika mabaraza hayo ya bunge hata baada ya kuondoka ofisini.

Kiongozi wa wengi wa chama cha Republic katika baraza la senate Mitch McConnell ameondoa uwezekano wowote wa baraza hilo kuandaa kikao cha dharura kilichoitishwa na kiongozi wa wachache Chuck Schumer.

Miongoni mwa watu waliovamia majengo ya bunge Marekani Januari 6, 2021.Picha: Douglas Christian/Zumapress/picture alliance

Kwenye taarifa iliyotolewa baada ya baraza la wawakilishi kupitisha mashtaka ya kumvua madaraka Trump, McConnel amesema kuwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za seneti katika mashtaka ya kumvua rais madaraka, ni wazi kuwa hakuna muda wa kutosha kuwezesha hayo kufanyika kwa kabla ya rais mteule Joe Biden kuapishwa.

soma pia: Twitter yaifunga akaunti ya Rais Trump

Ameongeza kuwa hata kama mchakato ungeanza wiki hii, maamuzi ya mwisho hayawezi kufikiwa kabla ya hatamu ya rais Trump kumalizika.

Wademocrat katika seneti wazungumziaje mashtaka dhidi ya Trump?

Ikiwa mchakato huo katika baraza la seneti utaanza baada ya Januari 20, basi Warepublic hawatakuwa na udhibiti wa seneti.

Kwenye taarifa, Chuck Schumer amekaribisha hatua ya kupitishwa kwa mashtaka ya kumvua Trump madaraka katika baraza la wawakilishi. Amesema haijalishi ni lini mchakato huo utamalizika kwenye seneti, jambo lililo wazi ni kwamba kutakuwa na mashtaka ya kumvua Trump madaraka katika baraza la seneti.

Viongozi duniani walaumu uvamizi wa majengo ya bunge na seneti nchini Marekani

01:59

This browser does not support the video element.

Schumer ameongeza kuwa baraza la seneti halitapiga kura tu dhidi ya Trump kuhusu makosa makubwa ya jinai, lakini pia ili kumzuia kuwania tena urais.

Trump ashutumu vurugu zilizofanyika Capitol Hill

Baada ya mashtaka dhidi yake kupitishwa, Trump ametoa ujumbe kupitia kanda ya video akishutumu vurugu za wiki iliyopita na kusema alisikitishwa na tukio hilo na kwamba hakuna mfuasi wake anayeunga mkono machafuko. Hata hivyo Trump hakuzungumzia hata kidogo yaliyopitishwa katika bunge la seneti.

Usalama umeimarishwa katika mji wa Washington kuelekea kuapishwa kwa Biden, hasa baada ya shirika la upelelezi FBI kuonya kuhusu mipango ya kufanyika maandamano katika miji yote mikuu ya majimbo ya Marekani.

(DW, AP)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW