Bunge la Poland lapiga kura kuidhibiti mahakama
19 Julai 2017Wabunge kutoka chama tawala cha kihafidhina, PiS, na washirika wao kwenye serikali ya mseto waliupitisha mswaada huo uliposomwa kwa mara ya kwanza jana na sasa kamati ya bunge inatazamiwa kuujadili kwa haraka na yumkini kuuridhia.
Kwa kura hii ya leo, bunge limechukuwa njia ya mkato kuelekea udhibiti wake dhidi ya mahakama kwa kuikabidhi kamati ya sheria na haki za binaadamu jukumu la kupitia na kisha kutoa maoni yake juu ya rasimu ya sheria hiyo. Kimsingi, hatua hii inawapa wanasiasa, na sio wanasheria, nguvu za kuwateuwa majaji wa Mahakama ya Juu na pia kuupanga upya muundo wa mahakama hiyo.
Usiku wa kuamkia leo, maelfu ya waandamanaji wa upinzani walikusanyika nje ya viwanja vya bunge, wakipinga kupitishwa kwa sheria hiyo. Jengo la bunge limekuwa likilindwa kwa vizuizi na walinzi wa serikali tangu majuzi, wakati waandamanaji hao walipoanza kumiminika katika mji mkuu wa Poland, na miji mingine nchini humo. Kiongozi wa maandamano hayo, Pawel Kasprzak, anasema kura hii inamaanisha kuuwa kabisa kanuni ya utenganishaji madaraka kwenye demokrasia ya Poland.
"Mgawanyo wa madaraka kwenye mikono mitatu ya utawala na uhuru wa mahakama umetiwa rehani hapa Poland. Kura hii inamaanisha kuwa waziri wa sheria sasa atawachaguwa majaji wa Mahakama ya Juu."
Mahakama ya Juu huitwa nchini Poland kwa jina la Baraza la Kitaifa la Mahakama na hapo Ijumaa iliyopita, bunge lilipitisha sheria ya kukomesha mihula ya majaji wa sasa wa mahakama hiyo na likajipa nguvu za kuwachaguwa majaji 15 kati ya 25 wa baraza hilo.
Umoja wa Ulaya wakasirishwa
Hayo yanajiri huku Umoja wa Ulaya ukitazamiwa kuongeza shinikizo dhidi ya serikali ya mrengo wa kulia nchini Poland hivi leo dhidi ya mswaada huu wa sheria ya Mahakama ya Juu. Msemaji wa Kamisheni ya Ulaya, Margaritis Schinas, amesema kuwa wanafuatilia kwa undani hali inavyoendelea Poland.
Kamisheni hiyo itakuwa na mazungumzo yake ya ngazi za juu leo, kabla ya Makamu wa Rais Frans Timmermans hajatoa tathmini yake kuhusu hali ya mambo ilivyo.
Kuelekea mkutano huo, Rais Andrzej Duda wa Poland ametaka kuwepo kwa maelewano kati ya upande wake unaowania kuidhibiti mahakama na upande wa upinzani, akisisitiza kwamba uteuzi wa majaji hao lazima upate uungwaji mkono na zaidi ya asilimia 60, sharti ambalo linaweza kufanya iwe tabu kwa chama chake tawala na washirika wake kupitisha wateule wao.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Josephat Charo