1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Tanzania lataka malipo ya Tundu Lissu yasimamishwe

Deo Kaji Makomba7 Februari 2019

Spika wa bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema ipo haja ya kusimamisha malipo yote ya Mbunge wa Singida mashariki Tundu Lissu kutokana na kwamba bunge hilo halina taarifa yoyote rasmi juu ya wapi alipo mbunge huyo.

Tansania Parlament in Dar es Salaam | Job Ndugai, Sprecher
Picha: DW/E. Boniphace

Bunge la Tanzania limesema kuwa ipo haja ya kusimamisha malipo yote ya Mbunge wa Singida mashariki Tundu Lissu kutokana na kwamba bunge hilo halina taarifa yoyote rasmi juu ya wapi alipo mbunge huyo.

Kauli hiyo ya bunge la jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, imetolewa leo hii mjini Dodoma na Spika wa bunge hilo, Job Ndugai wakati akijibu muongozo uliombwa na Mbunge wa jimbo la Geita vijijini Joseph Kasheku Msukuma aliyetaka kujua ni lini bunge hilo litasitisha mshahara na malipo mbalimbali ya Mbunge Tundu Lissu kwakuwa amekwishapona na kwa sasa amekuwa akizurura bila kuhudhuria vikao vya bunge vinavyoendelea hivi sasa.

Kulingana na Spika wa bunge la Tanzania Job Ndugai, wakati akijibu muongozo huo, amesema kuwa suala la mbunge Tundu Lissu linahitaji kuangaliwa kipekee na kwamba yale yaliyo ndani ya uwezo wake Spika atayafanya ikiwa ni pamoja na kusitisha malipo mbalimbali ya mbunge huyo kutokana na kwamba ofisi yake haina taarifa rasmi juu ya wapi alipo Tundu Lissu.

Tndu Lissu amekuwa akipata matibabu Ubelgiji kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.Picha: DW

Lakini wakati bunge likisema ipo haja ya kusitisha mishahara pamoja na malipo mbalimbali kwa mbunge Tundu Lissu, kwa upande wake mbunge huyo amekuwa akikana kuwa ofisi ya bunge haijagharamia matibabu yake tangu akutane na tukio la kushambuliwa kwa risasi kauli ambayo imepingwa na Spika Ndugai kwa kusema kuwa ofisi ya bunge imetumia mamilioni ya shilingi katika kugharamia matibabu ya mbunge huyo.

Mbunge Tundu Lissu yuko nchini Ubelgiji kwa zaidi ya mwaka mmoja akiendelea na matibabu baada ya kuvamiwa katika makazi yake mjini Dodoma na kisha kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana mnamo Septemba saba mwaka 2017.

Mwandishi: Deo Kaji Makomba, DW Dodoma.

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW