Bunge la Ufaransa kupiga kura ''kuitambua'' Palestina
28 Novemba 2014Pendekezo hilo ambalo ni la ishara tu lisilo na uzito kisheria, linatazamiwa kupitishwa bila upinzani mkubwa itakapopigiwa kura tarehe 2 Desemba. Chama cha kisoshalisti kilichoko madarakani ndicho kilichotoa pendekezo hilo.
Kura hiyo katika bunge la Ufaransa inakuja siku chache baada ya nyingine za aina hiyo katika mabunge ya Uhispania na Uingereza, ambayo yote yalipitisha mapendekezo ya kuutambua utaifa wa Palestina. Sweden ndio nchi pekee ya Ulaya ambayo imeutambua rasmi utaifa huo wa Palestina, tangu tarehe 30 Oktoba.
Chama cha kisoshalisti kilichowakilisha bungeni pendekezo hilo, kimezema ''kinatoa rai kwa serikali ya Ufaransa kutumia utambuzi wa taifa la Palestina kama nyenzo ambayo itasaidia kupata suluhisho la mwisho la mgogoro kati ya Israel na Palestina.
Ipo siku Ufaransa itaitambua Palestina
Ingawa kura ya bunge hilo haitakuwa hatua rasmi ya Ufaransa kuitambua Palestina, waziri mkuu wa nchi hiyo Laurent Fabius hivi karibuni aliliambia shirika la habari la Ufaransa , AFP, kwamba ipo siku Ufaransa itafikia uamuzi huo.
Mbunge wa chama cha kisoshalisti aliyewasilisha pendekezo hilo, Elisabeth Guigou, aliiambia AFP kwamba lengo ni kusisitiza kwamba suluhisho la mataifa mawili ndilo bora zaidi katika mgogoro wa Mashariki ya Kati.
''Tusipochukua hatua sasa, kuna hatari kwamba mgogoro huo utafika mahali ambapo kutakuwa na mzunguko wa visa vya ghasia ambao hauwezi kusimamishwa'' amesema mbunge Guigou, na kuongeza kuwa katika hali kama hiyo, mgogoro huo hautaishia tu kati ya Israel na Palestina, bali utalikumba kanda nzima.
Onyo la Netanyahu
Akizungumza kabla ya kura hiyo, waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliionya Ufaransa, akisema nchi hiyo ikiitambua Palestina itakuwa imefanya kosa kubwa sana.
Hapo jana, rais wa Ufaransa Francois Hollande aliwaambia waandishi wa habari mjini Paris, kwamba anaazimia kuitisha mkutano wa kimataifa utakaojaribu kutafuta suluhisho kwa mzozo kati ya Israel na Palestina. Hata hivyo hakusema mkutano huo utafanyika lini, wala kudokeza wadau watakaoalikwa.
Mbunge Elisabeth Guigou alisema Ufaransa ambayo inayo idadi kubwa zaidi ya wayahudi na ya waislamu kuliko nchini nyingine za Ulaya, inao uhusiano mzuri na Israel, na pia Palestina. Amesema kura ya leo haitaharibu uzani huo wa mahusiano, bali utathibitisha wito wa mara kwa mara kutaka pande hizo zitambuane, na haja ya kuwepo kwa usalama wa Israel.
Kwa kuzingatia mgawanyiko uliopo katika bunge la Ufaransa, inatarajiwa kwamba wabunge wa chama cha upinzani cha UMP watalipinga pendekezo hilo.
Ufaransa ilishuhudia maandamano makubwa ya kuiunga mkono Palestina wakati wa vita vya Gaza vilivyodumu kwa siku 50 majira ya joto yaliyopita.
Shirika linalotetea maslahi ya wayahudi, The Jewish Agency for Israel, limesema wayahudi wengi wameihama Ufaransa na kukimbilia Israel mwaka 2014, kuepuka kile ilichokiita ''mazingira ya chuki dhidi ya wayahudi''.
Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE
Mhariri:Josephat Charo