Bunge la Uganda lataka serikali kukomesha mateso kwa raia
8 Februari 2022Kwenye kikao cha alasiri ya Jumanne, wabunge wa pande zote mbili wameshtumu mienendo hiyo wakiwataka askari wa vyombo vya usalama kufahamu kuwa hata wao wakati mmoja watajikuta katika hali wanamowatia raia wenzao.
Kile ambacho kimewakera wabunge ni matamshi ya waziri wa usalama akikanusha kuwepo kwa vitendo hivyo na kwamba si sera ya serikali.
Huyo ni naibu Spika wa Bunge Anita Amongin akitamka kuwa hata yeye hana uwezo wa kukomesha vitendo vya watu kuteswa na vyombo vya usalama. Hii ni baada ya wabunge kadhaa kutoa vilio kwake kuingilia kati suala hilo ambalo wanasema linaitia Uganda katika fadhaa na fedheha.
Akijibu kwa niaba ya serikali, waziri wa nchi wa usalama Muruli Mukasa amekanusha kwamba vitendo vya kuwatesa watu kiasi cha kuwajeruhi na wengine kupoteza uwezo wao wa kuzaa watoto si
sera ya serikali. Amedai kwamba ikiwa vitendo hivyo vinafanyika basi wanaowajibika ni askari binafsi wala si taasisi za vyombo vya usalama.
Kiongozi wa upinzani Mathias Mpuuga amelitaka bunge kupiga kura ya kumfuta kazi waziri wa usalama Jim Muhwezi kwa kutowajibikia suala la watu kuteswa na kwa kiwango kikubwa kukiuka haki za binadamu.
Wadau mbalimbali ikiwemo umoja wa Ulaya wamekemea vikali vitendo vya mateso na kutaka wale wote ambao wanazuiliwa bila kufikishwa mahakamani waachiwe kwani watazidi kuchukuliwa kuwa wafungwa wa
kisiasa.