1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Uingereza kuidhinisha hoja ya May

Sylvia Mwehozi
19 Aprili 2017

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May amesema uchaguzi wa mapema mnamo Juni 8 mwaka huu badala ya kusubiri mwaka 2020 kutabadili hali ya mambo wakati wa mchakato wa mazungumzo na Umoja wa Ulaya na uchaguzi wa ndani.

UK | House of Lords
Picha: picture-alliance/empics/PA

Chini ya ratiba iliyopangwa, Uingereza inatarajiwa kuondoka rasmi Umoja wa Ulaya mnamo Machi 2019. Uchaguzi wa mapema Juni 8 unamaanisha Waziri Mkuu May hatokutana na wapiga kura tena hadi kufikia mwaka 2022 na kumpatia uwanja mpana wa ushawishi mwishoni mwa mazungumzo ya Brexit.

Wabunge wa Uingereza leo wanatarajiwa kuidhinisha mpango wa Waziri Mkuu May wa kufanya uchaguzi wa mapema baada ya kusema kwamba anataka kupunguza mgawanyiko wa kisiasa uliojitokeza juu ya safari ya taifa hilo kujiondoa Umoja wa Ulaya.

Bunge la Uingereza limepanga kuanzisha mjadala juu ya hoja hiyo mapema mchana wa leo na kufuatiwa na kura. Hoja ya kufanyika uchaguzi wa mapema Juni 8 inatarajiwa kupitishwa kwa urahisi kwa idadi ya theluthi mbili ya kura ya wengi inayohitajika ya wabunge 650.

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: Reuters/T. Melville

May amesema "Uingereza inaondoka Umoja wa Ulaya na hakuna kurudi nyuma. Na tukitizama mbele, serikali inayo mipango sahihi ya kujadiliana juu ya mahusiano mapya na Umoja wa Ulaya. Tunataka ushirikiano wa kina na muhimu kati ya Umoja wa Ulaya iliyo imara na Uingereza iliyo huru kuelezea njia zake yenyewe kwa ulimwengu."

Chama kikuu cha upinzani cha Labour kimeukaribisha wito wa May wa kufanyika uchaguzi wa mapema, hiyo ikimaanisha kwamba May atapata uungwaji mkono wa kura zinazohitajika katika bunge la juu ili uchaguzi uweze kufanyika.

Utafiti wa kura za maoni unapendekeza kwamba chama cha Waziri Mkuu May cha Conservative kinaongoza dhidi ya kile cha Labour, kama kilivyoandikwa kicha cha habari katika gazeti la Times la leo Jumatano, "May kuongoza kwa kishindo katika uchaguzi".

Gazeti hilo limenukuu taarifa ziilizokusanywa na shirika la kimataifa la utafiti wa intaneti lenye makao makuu Uingereza la YouGov ambalo limependekeza kwamba chama cha Conservatives wako katika nafasi nzuri ya kushinda kwa wingi viti 114 katika bunge la juu katika uchaguzi wa Juni 8.

Bendera za Uingereza na ile ya Umoja wa UlayaPicha: Getty Images/AFP/D. Leal-Olivas

May alisema hapo jana kwamba alikuwa akisita kutangaza mipango ya uchaguzi uliopangwa kufanyika mwaka 2020, lakini akaamua kwamba ilikuwa ni muhimu kuwazuia upinzani kuhatarisha mikakati yake juu Brexit.

Hata hivyo alivishutumu vyama vya upinzani vya Labour na vile vya kiliberali pamoja na chama cha taifa cha Scotland cha SNP na bunge la juu, ambalo wawakilishi wake si wa kuchaguliwa kwa kucheza "danadana za kisiasa" ambazo zingechelewesha mipango yake ya Brexit.

Baadhi ya wachambuzi wamehoji malengo ya May ya kupunguza upinzani wa kisiasa wakisema hiyo ni lazima ikubalike kama sehemu ya demokrasia iliyokomaa.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/Reuters/DPA

Mhariri: Josephat Charo