Bunge la Uingereza laidhinisha mchakato wa Brexit
14 Machi 2017Baada ya wiki kadhaa za mabishano, hatimaye bunge la Uingereza limempa waziri mkuu wa Uingereza Theresa May mamlaka ya kuanzisha mchakato wa kujiondoa kwenye Umoja huo ujulikanao kama Brexit kwa kutumia ibara ya 50 ya mkataba wa Lisbon ambayo inaashiria kuanza kipindi cha miaka miwili cha mchakato wa kujiondoa kwenye mkataba huo.
Mswada huo sasa unasubiri kuridhiwa na Malikia Elizabeth wa pili ili uwe sheria hatua ambayo inatarajiwa kukamilika Jumanne (14.03.2017) na hivyo kumpa rasmi Waziri Mkuu Theresa May mamlaka ya kuanzisha mchakato huo wakati wowote. Hata hivyo licha ya Waziri Mkuu Theresa May kusema kuwa ataanzisha rasmi utaratibu wa kawaida kuhusiana na hatua hiyo kufikia mwishoni mwa mwezi huu lakini bado hajasema lini hasa anatarajia kuanzisha rasmi mchakato huo ingawa kuna taarifa kuwa serikali ya Uingereza inatarajia kuanzisha mchakato huo baada ya mkutano wa kilele utakaofanyika Machi 25 katika maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Ulaya.
Scotland yataka kuitishwa kura ya pili ya maoni kuhusiana na Brexit
Ushindi huo wa serikali ya waziri mkuu Theresa May ulitiwa doa kufuatia kauli iliyotolewa na Waziri Kiongozi wa Scotland Nicola Sturgeon kutaka paitishwe kura ya pili ya maoni, kuhusu Scotland nayo kujitoa katika Muungano unaounda Uingereza. Muungano huo mbali na Scotland unazijumuisha England, Wales na Ireland kaskazini. Kauli ya Sturgeon inaashiria kuibuka kwa mvutano kuhusiana na mchakato huo wa Brexit.
Onyo lililotolewa na Umoja wa Ulaya kuwa Uingereza itakabiliana na masharti magumu katika hatua hiyo ya kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya nayo pia imeongeza mashaka juu ya mchakato huo.
Wakati huohuo hatua hiyo ya Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya imeibua hofu Ireland ya Kaskazini kuwa huenda ikasababisha kurejesha upya masharti magumu yanayohusiana na masuala ya forodha kati ya pande hizo mbili.
Waziri Mkuu Theresa May amelikosoa wazo la Scotland kuitisha upya kura ya maoni kudai kuwa huru, akisema wascotland wengi hawakubaliani na kuitishwa upya kwa kura hiyo huku pia akionya kuwa hatua hiyo itaibua mashaka na mgawanyiko.
Serikali ya Uingereza ina uwezo wa kuzima hoja hiyo ya waziri kiongozi wa Scotland lakini hata hivyo kufanya hivyo kunaweza kuongeza nguvu juu ya hisia za utaifa ndani ya Scotland.
Katika kura ya kwanza ya maoni iliyofanyika mwaka 2014, aslimia 55 ya wascotland walipiga kura kupinga kutengana na Uingereza ingawa kura ya maoni inaonyesha kuwa kura yoyote ya maoni itakayoitishwa upya itaonesha kukaribiana ambapo hatua ya Scotland kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya inaweza kuwa sababu kuu ya matokeo hayo.
Wakati wa kura ya kuamua Uingereza kusalia au kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya asilimia 62 ya wapiga kura wa Scotland walipiga kura kubakia kulinganisha na asilimia 48 ya waingereza wote waliopiga kura hiyo, lakini matokeo ya kura ya jumla za Uingereza nzima, yakaunga mkono kujitoa katika Umoja wa Ulaya.
Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE/ RTRE
Mhariri : Mohammed Abdul-rahman