1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUingereza

Bunge la Uingereza launga mkono mkataba wa baada ya Brexit

Saleh Mwanamilongo
23 Machi 2023

Wabunge wa Uingereza wamepiga kura kwa wingi kuunga mkono makubaliano ya Waziri Mkuu Rishi Sunak na Umoja wa Ulaya juu ya kanuni za biashara za baada ya Brexit zitakazotumika huko Ireland Kaskazini.

England Premierminister Rishi Sunak
Picha: ROGER HARRIS/UK PARLIAMENT/AFP

Wabunge 515 miongoni mwa 544 walipiga kura ya ndio, ili kuunga mkono makubaliano, ambayo yameundwa kusuluhisha mzozo wa kibiashara baina ya Uingereza na Umoja wa Ulaya. Lakini waziri Mkuu Rishi Sunak alikabiliwa na uasi kutoka kwa wabunge 22 wa chama chake  cha Wahafidhina, wakiwemo watangulizi wake wawili wa haraka. Mawaziri wakuu wa zamani Boris Johnson na Liz Truss wote walipiga kura ya kupinga mpango huo mpya.

Johnson, ambaye aliiongoza Uingereza kuondoka kwenye Umoja wa Ulaya, Brexit mnamo 2020, alisema mpango huo ulikuwa haukubaliki kwa sababu uliweka baadhi ya sheria za EU kufanya kazi Ireland ya Kaskazini, ukizuia uwezo wa Uingereza kujitenga na sheria za Umoja wa Ulaya.

Kundi la wabunge wenye msimamo mkali wa chama cha Conservative wanaojulikana kama Kundi la Utafiti la Ulaya pia lilisema linapinga itifaki hiyo. Serikali ilishinda kura kwa urahisi kwa kuungwa mkono na Chama cha Labour na makundi mengine ya upinzani, pamoja na wabunge wengi wa chama cha Conservative.

''Mkataba hulinda nafasi ya Irland Kaskazini katika muungano wetu''

Picha: PRU/AFP

Kabla ya kura ya Jumatano, waziri Mkuu Sunak alisema makubaliano hayo yalikuwa mpango mzuri kwa watu, familia na biashara za Ireland ya Kaskazini.

''Mkataba wa Windsor hurejesha usawa wa Makubaliano ya Belfast kuhusu Irland Kaskazini , hulinda nafasi ya Ireland Kaskazini katika muungano wetu. Inarejesha mamla ya kitaifa. Na kwa sababu hizo zote, nimefurahiya kwamba mkataba umepata uungwaji mkono mkubwa kama huu.Tutautekeleza sasa na kuhakikisha kwamba tunaweza kutazamia mustakabali mwema na bora zaidi wa Ireland Kaskazini.", alisema Sunak. 

Iwapo mkataba huo utaridhiwa na wanasiasa wa Ireland Kaskazini itakuwa hatua muhimu ya kusawazisha msuguano mkubwa uliokuwepo kati ya Brussels na serikali mjini London tangu Uingereza ilipojitoa rasmi kutoka Umoja wa Ulaya mwaka 2020.

Kupatikana makubaliano baina ya Uingereza na Umoja wa Ulaya kunahitimisha mwaka mzima wa majadiliano juu ya kile kinachofahamika kama "Itifaki ya Ireland Kaskazini".

Boris Johnson ajitetea kuhusu kashfa ya 'Partygate'

Huku hayo yakijiri, Waziri Mkuu wa zamani wa Boris Johnson amekanusha kuwa alilidanganya bunge la Uingereza kuhusu kashfa inayofahamika kama Partygate. Johnson jana alifika mbele ya Kamati ya Bunge kujitetea katika uchunguzi ambao huenda ukaamua hatima yake kisiasa. Kama kamati hiyo itaamua kuwa Johnson alilidanganya bunge kuhusu sherehe zilizoandaliwa ofisini mwake, huenda ikapendekeza kutimuliwa kwake bungeni na hata akapoteza kiti chake.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW