Bunge la Ujerumani kujadili ulinzi wa Mahakama ya Katiba
10 Oktoba 2024Pendekezo hilo lililowasilishwa na serikali ya muungano ya Kansela Olaf Scholz na chama cha upinzani cha Christian Democratic Union CDU, linalenga kuainisha ulinzi kwa mahakama hiyo katika katiba ya Ujerumani.
Hapo Jumatano, waziri wa haki Marco Buschmann aliashiria kuliunga mkono pendekezo hilo katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Ujerumani ARD.
"Tumeona nchini Poland na Hungary, mbinu zinazotumika kulemaza, kuharibu na kuzuia uhuru wa mahakama za katiba," alisema Buschmann.
Kwa sasa mahakama hiyo inaweza kufanyiwa mabadiliko endapo pendekezo la mabadiliko litapata uungwaji mkono wa wengi katika bunge la Ujerumani, Bundestag. Kwa upande mwengine katiba, inaweza kufanyiwa mageuzi tu endapo kutakuwa na uungwaji mkono wa thuluthi mbili katika mabunge yote.
Katika mpango huo mpya uliopüendekezwa, majaji watapewa muhula wa miaka 12 wa kuhudumu na watatakiwa kustaafu watakapofikia umri wa miaka 68, hilo likiwa litajumuishwa katika katiba.
Lakini Buschmann katika mahojiano menzine na shirika la habari la Ujerumani la Funke, ametahadharisha kwamba kupambana na wanasiasa wa siasa kali, si jukumu la kikatiba tu bali pia la kisiasa.