Schäuble Griechenland Hilfe
10 Juni 2011Bunge la Ujerumani leo limeunga mkono mpango wa pili wa kuisaidia Ugiriki kukabiliana na madeni yake makubwa .
Mpango huo umepitishwa na wabunge wengi baada ya waziri wa fedha bwana Wolfgang Schäuble kuupigia debe na kuhakikisha kwamba watu binafsi pia watashiriki.
Waziri Schäuble aliwaambia wabunge leo kwamba hatua za haraka zinahitajika ili kuisaidia Ugiriki . Waziri huyo amesema hali ni ya kutisha kwa Ugiriki na kwa Ulaya. Ametahadharisha kwamba ikiwa Ugiriki itashindwa kuyapila madeni yake, Ulaya yote itakuwa hatarini. Waziri huyo alisisitiza kwa wabunge ,ulazima wa kuisaidia Ugiriki ili isishindwe kulipa sehemu ya deni lake mnamo mwezi wa julai. Lakini waziri Schäuble amesisitiza kuwa Ugiriki inapaswa kwanza kuchukua hatua zaidi ili kuirekebisha bajeti yake.
Waziri Schäuble ameeleza kuwa ikiwa mtu anakopa kwa muda mrefu kama jinsi Ujerumani ilivyofanya basi hataweza kukwepa hatua za kufanya marekebisho. Waziri huyo amesema kuwa mgogoro wa uchumi nchini Ugiriki ulikuwa wa kina kirefu kuliko ilivyotarajiwa.
Hata hivyo amesema zipo ishara za kwanza za matumaini nchini Ugiriki zinazostahili kuungwa mkono. Lakini waziri Schäuble amesisitiza kuwa, tofauti na hatua ambazo zimechukuliwa hadi sasa, mpango wa safari hii wa kuisaidia Ugiriki utalazimu kuwashirikisha watu binafsi wenye dhamana za nchi hiyo. Ameeleza kuwa endapo patakuwapo mashaka juu ya uwezo wa Ugiriki, kulipa madeni yake, " basi kushiriki kwa sekta binafsi katika kulitatua tatizo ni jambo lisiloweza kuepukika"
Akiwahutubia wabunge leo waziri wa fedha wa Ujerumani bwana Schäuble alifafanua wajibu wa Ujerumani katika juhudi za kuutatua mgogoro wa sarafu ya Euro kutokana na Ujerumani kuwa nchi yenye nguvu kubwa za kiuchumi kuliko nyingine yoyote barani Ulaya.
Katika hotuba yake bungeni bwana Schäuble alisisitiza wajibu huo barani Ulaya na duniani kote. Schäuble alitamka kuwa dunia nzima itanufaika ikiwa sarafu ya Euro itakuwa imara, na hasa kutokana na matatizo yaliyopo katika sehemu nyingine za dunia.
Mwandishi/Stützle, Peter/DW-Intern/
Tafsiri/Mtullya Abdu/
Mhariri/Othman Miraj