1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Ulaya laitangaza Urusi kuwa taifa la ugaidi

23 Novemba 2022

Bunge la Ulaya limepiga kura kuitangaza Urusi kuwa "taifa linalofadhili ugaidi", likiwatuhumu wanajeshi wake kwa kufanya ukatili kwenye vita vyao nchini Ukraine huku Kyiv ikiupongeza uamuzi huo.

Straßburg EU-Parlament Rede Josep Borrell
Picha: FREDERICK FLORIN/AFP

"Mashambulizi ya makusudi na ukatili unaofanywa na Jamhuri ya Shirikisho la Urusi dhidi ya raia nchini Ukraine, uharibifu wa miundombinu inayotumiwa na raia na uvunjaji mwengine mkubwa wa haki za binaadamu na sherika za kimataifa, ni sawasawa na vitendo vya ugaidi. Bunge hili linaitambua Urusi kama taifa linalofadhili uaidi na kama taifa linalotumia njia za ugaidi." Ilisema sehemu ya azimio lililopitishwa mchana wa Jumatano (Novemba 23) mjini Strasbourg.

Licha ya kuwa kwake ishara kubwa kisiasa, hata hivyo, hatua hiyo ya wabunge wa Ulaya mehaina mashiko yoyote ya kisheria, na ndio maana wabunge hao wamezitaka serikali za mataifa 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya kuchukuwa maamuzi kama hayo.

Serikali ya Ukraine imekuwa ikiitaka jamii ya kimataifa kuitangaza Urusi kuwa "taifa la kigaidi" kutokana na uvamizi wake dhidi ya nchi hiyo, na hapana shaka uamuzi wa bunge mjini Strasbourg utaikasirisha Moscow. 

"Urusi lazima itengwe kwenye viwango vyote na iwajibishwe ili ikomeshe sera yake ya muda wote ya ugaidi dhidi ya Ukraine na kote ulimwenguni." Alisema Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine aliipongeza hatua hiyo.

Umoja wa Ulaya hauna mfumo wa kuanzisha azimio hilo

Bunge la Ulaya laitangaza Urusi kuwa taifa la kigaidi.Picha: Jean-Francois Badias/AP Photo/picture alliance

Kinyume na Marekani, ambayo tayari imeshaweka bayana nia yake ya kuitangaza Urusi kuwa taifa la kigaidi, Umoja wa Ulaya hauna mfumo wa kisheria wa kutangaza hatua hiyo.

Ikitekelezwa, hatua hiyo itapelekea vikwazo zaidi na inayoweza kuwaondolea viongozi wa Moscow kinga waliyonayo.

Azimio hilo, lililoungwa mkono na wabunge 494 dhidi ya 58 waliolipinga, linautaka Umoja wa Ulaya kuunda mfumo wa kisheria ili kuchukuwa hatua kama hiyo na kuiweka Urusi kwenye orodha ya ugaidi.

Mbunge Andrius Kubilius wa Lithuania, ambaye ndiye aliyeongoza kampeni ya kupatikana kwa azimio hilo amesema wanausema ukweli kama ulivyo.

"Urusi sio tu ni taifa linalofadhili ugaidi, lakini pia ni taifa linalotumia mbinu za kigaidi. Kwa bunge hili kutambuwa ukweli huo ni kutuma ujumbe wa wazi wa kisiasa. Ulaya na watu wa Ulaya hawataki kusalia goigogi, pale jirani yao mkubwa anapovunja vigezo vyote vya kibinaadamu na kimataifa." Alisema mbunge huyo. 

Wabunge kwenye nchi kadhaa za Ulaya mashariki wameshapiga kura kulaani "ugaidi" wa Urusi.

Tangu Rais Vladimir Putin alipoamuru vikosi vyake kuivamia Ukraine mwezi Februari, Umoja wa Ulaya umeshaweka awamu nane za vikwazo dhidi ya usafirishaji wa mafuta na maafisa wa juu wa Urusi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW