Bunge la Ulaya lamtunukia Mchina Hu Jai tuzo ya amani ya Sakharov.
24 Oktoba 2008Tuzo ya amani ya Sakharov ambayo hutolewa na bunge la Ulaya, mwaka huu amaetunukiwa mwanaharakati wa haki za binaadamu nchini China Hu Jia . Tuzo hiyo imepewa jina hilo kwa heshima ya aliyekua mpigania haki za binaadamu katika Urusi ya zamani mtaalamu wa Fizikia hayati Profesa Andrei Sakharov,aliyefariki Desemba 14, 1989.
Lakini tayari uamuzi huo umezusha malalamiko ya serikali ya China, huku Marekani ikiitaka imuachie huru mwanaharakati huyo aliye gerezani tangu mwezi Aprili mwaka huu.
Bunge la Ulaya lilimtaja mwanaharakati huyo wa haki za binaadamu nchini China Hu Jia mwenye umri wa miaka 35 kuwa mshindi wa mwaka huu 2008 wa tuzo ya amani ya Sakharov,ikiwa ni siku moja kabla ya mkutano wa kilele baina ya nchi za Asia na Ulaya mjini Beijing, licha ya shinikizo kutoka China ambayo imelaani hatua hiyo ikisema " ni uingiliaji mkubwa wa mambo yake ya ndani."
Hu alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu na miezi mitano jela na mahakama ya Bejing, na mwaka mmoja wa kunyimwa haki yake ya kisiasa. Wakati wa hukumu hiyo jaji alisema mwanaharakati huyo aliuhujumu mfumo wa kisiasa na kijamii wa China na kuchochea kulihujumu taifa, jambo ambalo kwa sheria ya China ni kosa.Mwanaharakati huyo bado yuko gerezani.
Muda mfupi baada ya Hu kutangazwa mshindi wa tuzo hiyo ya Sakharov na bunge la ulaya, Marekani ilisema inatumai China itamuachia huru mpinzani huyo.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani Gordon Duguid alisema nchi yake itaendelea kushirikiana na wengine katika jumuiya ya kimataifa, kuishajiisha China iheshimu haki za binaadamu kwa misingi inayokubalika kimataifa. Akaongeza,"hakuna anayepaswa kuwekwa gerezani kwa sababu ya kutoa maoni yake , au kupigania maisha bora ya raia wenzake."
Iikijibu shutuma hizo na nyenginezo, Shirika la habari la China Xinhua ilisema Hu yuko gerezani kwa kulihujumu Taifa.
Kandoni mwa hayo, wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani pia imeitaka China kumuachia mara moja padiri Zhang Minxuan ambaye inaripotiwa alikamatwa kusini magharibi mwa China na wanawe wawili wa kiume kupigwa na Polisi mjini Beijing.
Katika barua kwa Waziri wa mambo ya nchi za nje Condoleezza Rice, wabunge wa Marekani Frank Wolf na Christopher Smith walisema padiri Zhang alikamatwa tarehe 16 mwezi huu na siku tatu baadae polisi wakamtia nguvuni mkewe, ambaye aliwahi pia kukamatwa hapo awali kabla ya michezo ya Olimpiki mjini Beijing.
Padiri huyo anayeitwa jina la utani"baiskeli," kutokana na kusafiri kwake kote nchini China akigawa biblia na kuhubiri ni miongoni mwa viongozi maarafu wa kanisa nchini China.