Bunge la Ulaya lapitisha sheria kuhusu uhamiaji
26 Machi 2026
Kura hiyo ya leo inaruhusu wabunge wa Umoja wa Ulaya kuingia katika mazungumzo na nchi wanachama ili kukamilisha sheria hiyo ya uhamiaji.
Maamuzi hayo tata, yaliungwa mkono na wabunge 389 wa Umoja huo, huku 206 wakiyapinga na 32 wakijizuia kupiga kura.
Iwapo itaidhinishwa, sheria hiyo huenda ikawezesha kuanzishwa kwa vituo vya kuwapokea wahamiaji waliokataliwa nje ya Umoja huo wa Ulaya.
Marekebisho hayo pia yanalenga kuwapa fursa waomba hifadhi waliokataliwa kuondoka katika Umoja huo kwa hiari.
Chini ya sheria hiyo, waomba hifadhi waliokataliwa watalazimika kushirikiana katika kurejeshwa makwao.
Wahamiaji watakaokataa kufanya hivyo wanaweza kukabiliwa na adhabu, ikiwa ni pamoja na kupunguzwa kwa msaada kwao ama pia kupokonywa hati zao za kusafiria.