1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Ulaya lasimamisha makubaliano ya biashara na China

Daniel Gakuba
21 Mei 2021

Bunge la Ulaya limesimamisha kuidhinisha makubaliano ya uwekezaji baina ya umoja huo na China, hadi pale China itakapoondoa vikwazo ilivyowawekea wanasiasa wa Umoja wa Ulaya, hatua inayozidisha mzozo kati ya pande hizo

China Währung
Picha: Nicolas Asfouri/AFP

Katika kura iliyopigwa jana katika Bunge la Ulaya mjini Brussels, wabunge 599 walikubaliana na hoja ya kusimamisha kuidhinishwa kwa makubaliano hayo ya uwekezaji yaliyofikiwa mwezi Desemba baina ya wajumbe wa Umoja wa Ulaya na China, baada ya miaka saba ya majadiliano. Wabunge 30 tu walipinga, huku wengine 58 wakijizuia kupiga kura. Makubaliano yenye thamani kubwa yananuia kuyapa makampuni ya Ulaya fursa sawa kwenye soko la China, huku China ikipata hadhi ya kuwa mshirika wa kuaminiwa.

Soma zaidi: Ulaya na China zakutana Ubeligiji

Matatizo yalijitokeza mwezi Machi mwaka huu baada ya China kuwawekea vikwazo wanasiasa 10 wa Umoja wa Ulaya, pamoja na vikundi kadhaa vya wataalamu na taasisi za kidiplomasia za Ulaya. China ilikuwa ikijibu vikwazo vilivyowekwa na nchi za magharibi dhidi ya maafisa wake, ziliowatuhumu kuhusika na ukandamizaji dhidi ya jamii ya wachache ya Uyghur katika jimbo la Xinjiang kaskazini magharibi mwa China.

China na Umoja wa Ulaya walifikia makubaliano ya uwekezaji mwezi Desemba, 2020Picha: Johanna Geron/AP/picture-alliance

China yapiga mahesabu vibaya?

Kwenye orodha ya wanasiasa wa Ulaya waliowekewa vikwazo na China wamo wabunge watano wa Bunge la Umoja wa Ulaya, miongoni mwao akiwa Reinhard Buetikofer kutoka Ujerumani, ambaye amesema kwa kuweka vikwazo hivyo, China ilipiga mahesabu yake vibaya.

Buetikofer amesema ''badala ya kuwawekea vikwazo maafisa wa Ulaya, China ingepaswa kujifunza kutokana na makosa yake na kujirekebisha.''

Soma zaidi: Maelfu ya Wauighur wanafanyishwa kazi kwa lazima 

Wabunge wa Ulaya wanatoa hoja ya kwamba wakati vikwazo vilivyowekwa na Uingereza na Marekani dhidi ya China vilikuwa katika mipaka ya mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, vikwazo vya China dhidi ya maafisa wa Ulaya havikuwa na msingi katika sheria ya kimataifa.

Msemaji wa wizara ya nje ya China Zhao LijianPicha: picture-alliance/Kyodo

China yaitaka Ulaya kuacha kuongozwa na hisia

China kwa upande wake inashikilia kuwa haijafanya kosa lolote. Katika mkutano wa kila siku na waandishi wa habari, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Zhao Lijian amesema ingekuwa bora kama Ulaya ingefanya maamuzi ya kutumia akili badala ya kutawaliwa na hisia, katika kulinda na kusimamia maslahi yake.

Soma zaidi: HRW: China ni kitisho kikubwa kwa haki za binadamu

Hali kadhalika, Ubalozi wa China katika Umoja wa Ulaya umesema makubaliano ya uwekezaji ambayo bunge la Ulaya limeyasimamisha ni kwa manufaa ya pande mbele na sio ya upendeleo kwa China, na kutetea vikwazo vilivyowekwa na Beijing dhidi ya maafisa wa Ulaya.

Wanadiplomasia wa Ulaya wanasema hakuna upande wowote unaofaidika kutokana na mkwamo huu kati, kwa sababu kila upande, Umoja wa Ulaya na China, unazo faida nyingi katika makubaliano hayo.

 

rtre, afpe

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW