1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Ulaya na CIA

14 Februari 2007

Bunge la Ulaya huko Strassbourg limeidhinisha ripoti inayolaani vikali safari za ndege za siri zilizofanywa katika nchi 14 za Ulaya kuwasafirisha watuhumiwa ugaidi.

Bunge la Ulaya mjini Strassbourg, liliidhinisha jana ripoti ya mwisho inayolaani safari za ndege za siri za shirika la ujasusi la Marekani (CIA) juu ya anga la nchi kadhaa za Ulaya.Ripoti hiyo imezituhumu serikali za Ulaya na mashirika yao ya ujasusi kuridhia na hata kuuficha mpango wa safari hizo kupitia anga za nchi zao.

Bunge la Ulaya limearifu katika ripoti yake kwamba linalaani vikali safari hizo zilizotumiwa na Marekani katika vita vyake vya kupambana na ugaidi na kuvieleza kuwa si halali.Bunge la Ulaya isitoshe, linalaani zaidi kuziona serikali nyingi za Ulaya na mashirika yao kuridhia kutumiwa kwa misafara hiyo.Ripoti hii ilipitishwa bungeni mjini Strassbourg kwa wingi mkubwa.Wabunge 384 waliipigia kura ripoti hiyo kuiidhinisha na 256 waliipinga huku 74 hawakupiga kura spande wowote.

Wabunge wa Ulaya waliikosoa Itali na wakamuungamkono mshtaki wa serikali wa nchi hiyo aliedai kuwashtaki wamarekani 26 wengi wao inaaminiwa ni majasusi wa CIA pamoja na wataliana 6 kwa kuhusika na kutekwanyara 2003 kwa shehe mmoja wa kiislamu mjini Milan,Itali.

Wabunge walikataa mageuzi yaliopendekezwa na chama cha kihafidhina cha Ulaya kilichodai kuwa hakuna ushahidi wa kutosha kwamba serikali ya waziri-mkuu Silvio Berlusconi, ilijua kunyakuliwa kwa Sheikh Hassan Mustafa Osama Nasr, maarufu kwa jina la Abu Omar.

Bunge la Ulaya hatahivyo, halina mamlaka ya kisheria kukata shughuli kama hizo kwahivyo, laweza tu kutoa mapendekezo.

Mjumbe mmoja katika Bunge hilo Ignasi Guardans alinukuliwa kusema,

“Huwezi kuupiga vita ugaidi kwa vita vichafu tena kwa niaba yetu.”

Mjumbe wa chama cha kisoshalist Claudio Fava, alisema kuwa serikali nyingi za ulaya zilifumba macho.

Marekani inaungama kuwa ikiwasafirisha kisisiri washukiwa ugaidi lakini inakataa tuihuma za kuwatesa au kuwakabidhi mikononi mwa nchi zilizowatesa.

Ujerumani ambayo ndiyo mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Ulaya na mojawapo ya nchi 14 zilizokosolewa kuvumilia safari hizo za siri, iliwaambia wabunge kuchukua hadhari na baadhi ya tuhuma wanazotoa.

Kamishna wa Umoja wa Ulaya wa maswali ya sheria na salama, Franco Frattini akaongeza:

“Si jukumu la taasisi za Ulaya kutoa hukumu na adhabu bali ni kutafuta ukweli wa kilichofanyika.”

Frattini akigusia hapo uchunguzi wa kisheria na wa kibunge unaofanywa katika nchi kadhaa za Ulaya juu ya mkasa huu miongoni mwa nchi hizo- Ujerumani,Spian na Ureno.

Vikundi vinavyotetea haki za binadamu vimewataka wabunge wa Ulaya huko Strassbourg kutoilainisha ripoti iliotolewa katika kura ya jana juu ya ripoti hiyo.

Si chini ya safari za ndege 1,245 za shirika la kijasusi la Marekani (CIA) zilifanyika katika nchi za Ulaya au kupitia anga za nchi hizo mnamo muda wa miaka 4- kufuatia hujuma ya Septemba 11, 2001, nchini Marekani-ripoti iliarifu.