1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge Urusi laidhinisha unyakuzi wa majimbo manne ya Ukraine

4 Oktoba 2022

Rais Vladmir Putin atarajiwa kutia saini sheria ya kuyajumuisha rasmi majimbo manne ya Ukraine kuwa sehemu ya Urusi

Russland Moskau | Parlament
Picha: Sergei Fadeichev/TASS/dpa/picture alliance

Bunge nchini Urusi limeidhinisha unyakuzi wa majimbo manne ya Ukraine yaliyotwaliwa kimabavu kupitia mchakato ya kura ya maoni usiokuwa halali uliopingwa na nchi za Magharibi na Ukraine yenyewe na rais Putin anatarajiwa kutia saini kupitisha uamuzi huo.

Kufuatia hatua hiyo rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameondowa rasmi uwezekano wa kuwa na mazungumzi na Urusi akitowa tamko hilo leo Jumanne kwa kusema kwamba kufanya mazungumzo rais wa Urusi Vladmir Putin ni jambo haliwezekani tena baada ya uamuzi wake wa kuyanyakuwa majimbo hayo ya Ukraine.

Lakini kwa upande mwingine serikali ya Urusi imejibu kwa kusema kwamba itaisubiri Ukraine mpaka itakaporidhia kukaa chini kwa mazungumzo ya kuumaliza mgogoro,ingawa pia ikikumbusha kwamba huenda hilo halitofanyika mpaka nchi hiyo ya Ukraine itakapopata kiongozi mpya. Msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov amesema na hapa tunanukuu,

'' Tutasubiri rais abadili msimamo wake au tutasubitri kionghozi mpya atakayeingia madarakani ambaye atabadilisha msimamo wake kwa ajili ya maslahi ya watu wa Ukraine''

Picha: Alexei Nikolsky/AP Photo/picture alliance

Pigo kwa Urusi

Pamoja na hayo  imeripotiwa kwamba katika mji   muhimu wa mashariki mwa Ukraine wa Lyman, maiti za wanajeshi wa Urusi zimeshuhudiwa zikiwa zimetapakaa katika barabara za mji huo leo Jumanne ikiwa ni ushahidi wa mpambano mkali uliosababisha maafa kwa wanajeshi wa Urusi na kuonesha kushindwa kwa mara nyingine kwa jeshi la Urusi wakati likipambana kuendelea na vita kwenye maeneo iliyoyanyakua kwa mabavu wiki ilyopita kwa njia isiyokuwa halali.

Mwishoni mwa juma inaelezwa kwamba wanajeshi wa Urusi walijiondowa katika mji wa Lyman ambao ni mji muhimu wa kimkakati  uliokuwa ukitumiwa na wanajeshi wa Urusi kama njia kuu ya usafiri na kituo cha usafirishaji kuepuka kuzingirwa na vikosi vya Ukraine. Kukombolewa kwa mji huo kumeipa Ukraine nguvu kubwa ya kuendelea na mapambano yake kuingia ndani zaidi  kwenye majimbo hayo yaliyonyakuliwa na Urusi.

Picha: Evgeniy Maloletka/AP/picture alliance

Ikiwa ni siku mbili sasa zimepita bado miili ya wanajeshi wa Urusi inaelezwa kwamba imeendelea kubakia kwenye barabara za mji huo. Ukraine imeshachukua maiti za wanajeshi wake waliokufa kwenye uwanja wa vita katika mji huo wa Lyman.Wakaazi wa mji huo waliokuwa wamejificha kwenye mahandaki wamejitokeza na kuwasha moto mkubwa kwaajili ya kupika.Lakini pia inaelezwa kwamba hakuna huduma ya maji wala gesi katika mji huo ulioko kwenye jimbo la Donestk tangu mwezi Mei.Majumba chungunzima yameteketezwa.

Vikosi vya Ukraine vyasogea

Wanajeshi wa Ukraine sasa wamesogea na kufika umbali wa kukaribia mpaka wa jimbo jirani la Luhansk wakielekea Kreminna.Wakati huohuo rais wa Belarus Alexander Lukashenko wa ameituhumu Ukraine kwa kupeleka wanajeshi 15,000 katika eneo la mpakani kwa ajili ya kuweka ulinzi na kuendesha utafiti wa kijeshi ,matukio ambayo ameyaita ni uchokozi.Ikumbukwe kwamba Lukashenko mnamo mwezi Februari alimruhusu mshirika wake wa karibu Urusi kuitumia Belarus  kama kituo chake cha kijeshi kwa ajili ya uvamizi wake dhidi ya Ukraine.Hata hivyo rais huyo wa Belarus alijitokeza na kusema  nchi yake sio sehemu ya mgogoro na kwamba wanajeshi wake hawahusiki.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW