Bunge la Zimbabwe laanza mchakato wa kumuondoa Rais Mugabe
21 Novemba 2017Bunge la Zimbabwe limeanzisha mchakato wa kumuondoa kisheria Rais Robert Mugabe madarakani. Wabunge kutoka vyama mbalimbali vya kisiasa wamemtaka Mugabe mwenye umri wa miaka 93 kujiuzulu baada ya jeshi kuchukua udhibiti wa mamlaka wiki iliyopita na pia baada ya maelfu kwa maelfu ya waandamanaji kujitokeza barabarani kumtaka Mugabe kung'atuka.
Spika wa bunge la Zimbabwe Jacob Mubenda alitoa idhini ya vikao vya pamoja vya bunge na seneti kujadili hoja itakayopelekea mchakato wa kuondolewa madarakani Rais Robert Mugabe.
Mbunge wa chama tawala Monica Mutsvangwa ndiye aliyeiwasilisha hoja ya kumtaka Mugabe kuondolewa madarakani, kisha ikaungwa mkono na mbunge wa upinzani James Maridadi. Spika Mubenda amesema hoja hiyo kamwe haijawahi kutokea katika historia ya nchi hiyo tangu ipate uhuru.
Hayo yakifanyika, umati mkubwa wa waandamanaji ulikusanyika nje ya bunge la Zimbabwe kushinikiza Mugabe ajiuzulu.
Shinikizo zaidi dhidi ya Mugabe kutoka kwa maveterani wa vita vya ukombozi
Chama cha maveterani wa vita vya ukombozi wa nchi hiyo kimekuwa katika mstari w ambele kumshinikiza Mugabe kujiuzulu. Mwenyekiti wa chama hicho Christopher Mutsvangwa amesema Mugabe hana ushawishi hata ndani ya serikali yake na wakati wake wa kuondoka umetimia. Anaongeza kusema:
"Ikiwa hataondoka, tutawatolea mwito kwa mara nyingine Wazimbabwe warudi wamtimue. Tutawarudisha barabarani wote waliojitokeza Jumamosi, na wakati huu tutamuhimiza kila mtu ajitokeze ili kumuonesha kuwa Wazimbabwe wote walimtaka aondoke toka jana''
Wabunge kutoka vyama mbalimbali wamekuwa wakimtaka Mugabe mwenye umri wa miaka 93, ajiuzulu, baada ya jeshi kuchukua mamlaka na kumweka Mugabe katika kizuizi cha nyumbani, na baada ya maelfu kwa maelfu ya waandamanaji kujitokeza barabarani kumtaka Mugabe ajiuzulu.Wanamlaumu Mugabe kwa kuwa mzee hivyo kushindwa na majukumu, kumruhusu mke wake kuchukua mamlaka yake.
Marais Jacob Zuma na Joao Lourenco kuzuru Zimbabwe Jumatano
Katika tukio jingine, rais wa Angola Joao Lourenco amewaambia waandishi wa habari kuwa yeye na rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma wataelekea Zimbabwe kesho Jumatano kuushughulikia mzozo wa nchi hiyo. Hii ni baada ya viongozi hao kufanya mkutano nchini Angola leo, mkutano ambao pia ulihudhuriwa na viongozi wa Zambia na Tanzania.
Nayo serikali ya Botswana imechapisha kwenye mtandao, kile inachokiita kuwa barua wazi kutoka kwa Rais Ian Khama kumhimiza Robert Mugabe ajiuzulu. Katika kipindi cha nyuma, Khama amekuwa akimkosoa waziwazi jirani yake. Barua hiyo imemtaka kiongozi huyo wa Zimbabwe kuzingatia matakwa ya raia wa Zimbabwe na kufanya jambo la heshima- kujiuzu kwa khiari.
Punde baada ya Mugabe kumfuta kazi aliyekuwa makamu wake Emmerson Mnangagwa, Grace Mugabe alitizamwa kama mtu anayelenga shabaha ya kutaka kumrithi Mugabe. Hali hiyo ilisababisha mzozo ulioko kwa sasa pale jeshi lilipotangaza kuchukua madaraka.
Mchakato wa bunge wa kumuondoa Mugabe madarakani unajiri baada ya Mugabe kukataa kutangaza kujiuzulu kwa hiari wakati wa hotuba yake iliyopeperushwa kupitia televisheni siku mbili zilizopita.
Tayari chama tawala ZANU-PF kimemfuta Mugabe kama kiongozi wake, hata hivyo Mugabe amepuuzilia hilo.
Mugabe amekuwa madarakani kwa miaka 37.
Mwandishi: John Juma/AFPE/RTRE/APE/DPAE
Mhariri: Yusuf Saumu